UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kwamba bado una imani na Kocha Mkuu wa timu hiyo Cedric Kaze licha ya timu kushindwa kupata matokeo chanya ndani ya uwanja kwenye mechi za hivi karibuni.
Yanga mzunguko wa pili imeanza kwa kusuasua huku ikipewa presha kubwa kutoka kwa watani wao jadi Simba ambao kasi yao inazidi kuwa kubwa kila waingiapo ndani ya uwanja.
Mechi ya kwanza waliyocheza dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Nelson Mandela waliambulia sare ya kufungana bao 1-1 na walipocheza na Mbeya City ubao ulisoma 1-1.
Pia mchezo wake wa tatu wa mzunguko wa pili ilikubali sare ya kufungana mabao 3-3 jambo ambalo lilipeleka Uongozi wa Yanga kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wao Fredrick Mwakalebela kulalamika kwa kusema kuwa waamuzi wamekuwa wakiwanyima penalti na kutishia kujiweka kando ndani ya ligi.
Mchezo wao uliofuata dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 na kukusanya jumla ya pointi 49 ipo nafasi ya kwanza huku ikifuatiwa na Simba iliyo nafasi ya pili na ina pointi 45.
Imeweza kutinga hatua ya 16 bora kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ken Gold mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru.
Mshauri wa Yanga kuelekea kwenye suala la mabadiliko, Senzo Mbatha amesema kuwa wanatambua mwendo ulivyo na wana imani na Kaze.
"Tunaimani na Kaze na matokeo ambayo tunayapata tunaamini kwamba ni sehemu ya mchezo kwa kuwa ikiwa tutashinda iwe ni kwa mabao mengi ama moja kinachotazamwa ni ushindi.
"Mashabiki wasiwe na presha imani yetu ni kwamba kila kitu kitakuwa sawa na mambo yatakwenda kwenye utaratibu ambao tunahitaji hakuna haja ya kuwa na presha,"
Machi 4 ina kibarua cha kusaka ushindi mbele ya Coastal Union kwenye mchezo wa ligi utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.