Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 11 Aprili, 2021 ameondoka nchini kwenda Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Tanzania imeeleza kuwa Rais Samia akiwa Uganda atazungumza na mwenyeji wake Rais Yoweri Kaguta Museveni kwenye uwanja wa Ndege wa Entebbe.
Baada ya mazungumzo hayo ya faragha wawili hao watashuhudia utiaji saini mkataba kati ya Serikali ya Uganda na kampuni ya mafuta ya ghafi ya Afrika Mashariki (EACOP).
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda kwenda Tanga Tanzania itafanyika Ikulu ya mjini Entebbe.