UONGOZI wa Azam FC, umesema kuwa hawapo tayari kumuuza staa wao, Mzimbabwe, Prince Dube, kwenda Simba na badala yake ataendelea kubaki kikosini kwao.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu ziwepo tetesi za Simba kuwa kwenye mipango ya kumnasa mshambuliaji huyo anayeongoza kwa mabao Ligi Kuu Bara akiwa amepachika 12.
Taarifa zilizopo kwa sasa ni kwamba, hivi karibuni mshambuliaji huyo ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Azam, hivyo atakuwa hapo hadi 2024.Akizungumza na Spoti Xtra,Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema Dube hataenda timu yoyote hapa nchini, bali atabaki Azam.
Popat aliongeza kuwa, mshambuliaji huyo kama akiondoka Azam, basi atakwenda kucheza soka nje ya Tanzania.“Kwa kifupi Dube hatakwenda popote ndani ya nchi hii, ataendelea kubaki Azam.
“Dube kama akiondoka hapa Azam, basi atakwenda kucheza soka nje ya Tanzania na siyo kwenye klabu za hapa.
“Hizo timu zinazomtaka hata watoe dau kubwa kiasi gani, sisi Azam hatutalipokea, hivyo nao waende kutafuta wachezaji bora nje ya nchi kama sisi tulivyokwenda kumtafuta Dube,” alisema Popat.
Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam