MTENDAJI Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez, amesema kuwa moja ya vitu ambavyo vimefanya watishe kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) msimu huu ni uwezo wao wa kuwachambua wapinzani kabla ya kukutana nao.
Barbara alisema kwa msimu huu aliamua kuwekeza kwenye kutafiti wachezaji hatari wa timu pinzani na timu kwa jumla na ndiyo maana akamuajiri mtu maalumu kwa ajili ya kazi hiyo, huku mitandao ikiwa ni njia nyingine ambayo amekuwa akiitumia na kupata majibu chanya ambayo yanawasaidia.
Barbara alisema mpira ni sayansi kubwa ambayo inahitaji utafiti wa kina ili kupata kitu ambacho unakihitaji, ndiyo maana kuna wakati imekuwa rahisi kuona wachezaji kama Luis Miquissone na Clatous Chama kucheza kwenye mfumo fulani kulingana na utafiti waliofanya.
“Nilishawahi kusema sehemu fulani kuwa msimu huu mimi nimewekeza zaidi kwenye ‘analysis’ ili kuweza kubaini uwezo wa wapinzani na mchezaji gani hatari kwa mpinzani wetu, ndiyo maana niliajiri mtu wa kufanya hiyo kazi na wakati mwingi nilikuwa natumia mitandao.
“Mpira unaendeshwa na sayansi na unahitaji sayansi ili kuchambua masuala, kwa hiyo kwa kutumia analysis za mtu wetu, unaweza kujua namna ya kupanga na kuelekeza wachezaji wako wacheze namna gani, unaweza kumwambia Kapombe, Josh cheza hivi kwa sababu huyu unayekabana naye ni mtu wa namna gani,” alisema Barbara.
Simba wanajiandaa kuwakabili Al Ahly katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi utakaopigwa leo Ijumaa Aprili 9, 2021 nchini Misri. Wanakwenda kwenye mchezo huo wakiwa tayari wamefuzu hatua ya robo fainali wakiwa na alama 13 na kuongoza Kundi A.