Bodi ya Filamu yatakiwa kupeleka filamu TBC





Bodi ya filamu Tanzania imetakiwa kupeleka filamu zenye mafunzo mbalimbali kwenye kituo cha televisheni cha Taifa (TBC 1) ili kujenga jamii imara.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul ametoa rai hiyo wakati akizungumza na Menejimenti ya Bodi ya Filamu Tanzania wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Amesema siku hizi haoni filamu TBC 1, na kuitaka bodi hiyo kuangalia utaratibu wa kuonesha filamu katika televisheni hiyo.

Naibu Waziri Gekul ameongeza kuwa, miaka ya nyuma kulikua na filamu na tamthilia ambazo zilikua zina mafunzo kwa jamii lakini siku hizi hazionekani, ambazo zingeoneshwa zingekuwa na msaada mkubwa kwa jamii.

Ameiagiza bodi hiyo kuhakikisha zinaoneshwa katika televisheni za kulipia, lakini pia vituo vya televisheni vya bure.

Awali, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Edward Kilonzo alisema kuwa, bodi yake imefanikiwa kutetea haki za Wasanii wa hapa nchini.

Ametolea mfano. msanii mkongwe Marehemu Amri Athuman 'Mzee Majuto', ambaye familia yake ililipwa shilingi milioni 65, familia ya Steven Kanumba ililipwa shilingi milioni 15, Young D amelipwa shilingi milioni 20 kutokana na kazi zao za sanaa.

Kwa mujibu wa Kilonzo, filamu mbili za Tanzania zimefanikiwa kuoneshwa katika majumba ya sinema ya Afrika Mashariki.

Filamu hizo ni Nyala na Binti na filamu ya 'Decision' inakaribia kutoka na kuoneshwa katika mfumo huo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad