Meneja wa fedha wa kampuni ya Clouds Media Group, Issa Masoud amesema walitoa vielelezo vyote ikiwa ni pamoja na stakabadhi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kufuatia malipo ya Sh629.7 milioni kwa ajili ya matangazo ya tamasha la urithi mwaka 2018.
Masoud ametoa ufafanuzi huo leo Alhamisi Aprili 8, 2021 katika kipindi cha Traffik Jamz kinachorushwa na redio Clouds saa chache baada ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kueleza kuwa Clouds ililipwa kiasi hicho cha fedha lakini hakukuwa na risiti zozote za kielektroniki zilizotolewa kuthibitisha malipo husika.
Katika ripoti hiyo ya CAG, imeeleza kuwa televisheni ya Clouds walilipwa Sh629.7milioni na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Sh201.4 milioni kwa ajili ya kuonyesha matangazo ya tamasha hilo.
Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma CAG, Charles Kichere amesema kodi ya zuio ya Sh31 milioni na Sh10 milioni kutoka Clouds na TBC hazikukatwa kutoka katika malipo hayo.
"Wizara haikutimiza wajibu wake katika kukata hiyo kodi ya zuio, vilevile sikupewa ushahidi ukionyesha kuwa manunuzi ya huduma za matangazo kutoka TBC na Clouds yalipatikana kwa ushindani ulio sawa.”
“Pia nilibaini Sh487 milioni zilipelekwa kwenye taasisi saba kwa ajili ya utekelezaji wa tamasha hata hivyo hakukuwa na nyaraka zilizowasilishwa kwa wakaguzi kuthibitisha matumizi hayo,” amesema.