Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amesema kufuatia taarifa ya kuwepo kwa kimbunga cha Jobo katika Bahari ya Hindi, mkoa huo umeanza maandalizi ya kuchukua tahadhari kuhakikisha usalama wa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 24, 2021 Kunenge amesema ofisi yake kwa kushirikiana na halmashauri zote tano pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, wanaendelea kuchukua tahadhari muhimu.
Amesema Kituo cha Uratibu wa Maafa (EOC) kimehusishwa kwa ajili ya kuendelea na uratibu za taarifa za mwenendo wa kimbunga hicho zinazoendelea kutolewa na TMA .
"Vikosi mbalimbali Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Msalaba Mwekundu, taasisi kutoka huduma za afya, magari ya kubeba wagonjwa ,waratibu wa maafa wa halmashauri na taasisi nyingine wamejiandaa kwa maafa yatakayoweza kujitokeza,” amesema Kunenge.
Hata hivyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kasi ya kimbunga hicho kinachotarajiwa kupiga Pwani ya Bahari ya Hindi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia imeongezeka ambapo kinasafiri kwa kasi ya kilometa 20 kwa saa baharini.
“Kimbunga ‘Jobo’ kwa sasa kinasafiri kwa kasi ya kilometa 20 kwa saa baharini ambayo ni kasi kubwa kwa mwenendo wa vimbunga. Kutokana na kasi hiyo kubwa, kisiwa cha Mafia na maeneo jirani yanatarajiwa kuanza kupata mvua kubwa mapema zaidi leo jioni tarehe 24/04/2021”, imesema taarifa ya TMA
Aidha taarifa imesema kuwa kuanzia usiku wa kuamkia Jumapili Aprili 25, 2021 maeneo ya kusini mwa mikoa ya Pwani na Dar Es Salaam yanatarajiwa kupata mvua kubwa wakati maeneo mengine ya Lindi, Mtwara na kisiwa cha Unguja pia yanatarajiwa kupata vipindi vya mvua kubwa siku ya kesho Jumapili kwa baadhi ya maeneo.