Na Omary Mngindo, Kibaha.
DIWANI wa Kata ya Mbwawa Jimbo la Kibaha Mji Mkoa wa Pwani Judith Mluge, amewaomba wabunge wa majimbo ya Bagamoyo, Kibaha Mji, Kibaha Vijijini na Kisarawe kuendelea kuipigania barabara itokayo Makofia, Yombo, Mlandizi mpaka Mzenga.
Amewataja wabunge hao kuwa ni Muharami Mkenge (Bagamoyo), Silvestry Kona (Kibaha Mji), Michael Mwakamo (Vijijini) na Suleiman Jafo (Kisarawe) kuendelea kupigania barabara ya Makofia, Mlandizi mpaka Mzenga Kisarawe ambayo imekuwa changamoto kubwa.
Judith alitoa ombi hilo kwenye kikao cha Kamati ya siasa Kibaha Mji, ambapo alisema hali ya barabara hiyo ni mbaya, hivyo amewaomba wabunge hao kuendelea kuipigania ili ahadi ya ujenzi ianze haraka hatimae kuwakomboa wasafiri.
"Barabara yetu inapita katika majimbo hayo manne, pia umuhimu mkubwa kwani inawahudumia watu wanaotokea maeneo mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara za samaki na nyinginezo ambapo wenye vyombo vya usafiri wakilalamikia kuharibika, sanjali kupandisha nauli kipindi cha mvua" alisema Diwani huyo.
"Natambua waheshimiwa wabunge wetu wanaendelee kutupigania ili ahadi ya Serikali kuijenga barabara yetu kwa kiwango cha lami inafanikiwa, niwaombe waongeze kupambania bungeni ili Serikali kupitia Wizara iifanyiekazi kwani kwa miaka mingi tunateseka," alisema Judith.
Aliongeza kwamba kwa miaka mingi barabara hiyo imekuwa ikizungumzwa kuhusu ujenzi wake, lakini utekelezaji wake hauonekani huku akieleza kwamba katika ilani ya mwaka 2020/2025 imeonekana kuwepo kwa mkazo mkubwa, huku akiwaomba wabunge hao kuongeza msukumo serikani.
"Kwa miaka mingi wananchi wamesimamishwa wasiendeleze maeneo yao, ikiwemo nyumba kwa sababu tayari baadhi ya taratibu zikionesha kukamilika, niwaombe waheshimiwa wetu hawa waipiganie kwani wananchi wanateseka sana", alisema Mluge.