Baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kubainisha matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyokuwa inaongozwa na Dk Hamisi Kigwangalla, ameibuka kwenye mtandao wa kijamii na kuandika, “nitashtaki kwa Mungu, Wallahi!”
Kigwangalla alikuwa waziri katika wizara hiyo kuanzia Oktoba 7, 2017 hadi Novemba 2020 na Rais wa tano, Hayati John Magufuli hakumrudisha katika baraza lake la mawaziri.
Akiwa Waziri, Kigwangalla alianzisha tamasha la urithi pamoja na shindano la kupanda Mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuhamasisha utalii nchini sambamba na watu kupanda mlima huo mrefu Afrika.
CAG katika ripoti hiyo ameeleza kuwa shindano hilo lilitumia Sh172 milioni zilizotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kiasi cha Sh114 milioni na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) na kiasi cha Sh57 milioni zilizotolewa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). Alisema fedha hizo hazikuwa kwenye bajeti zao za mwaka wa fedha.
Katika majibu yake kuhusu kutajwa kwake huko kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Instagram, Kigwangalla amesema, “nitashtaki kwa Mungu, Wallahi!”
Baada ya kauli yake hiyo baadhi ya wa watu walitoa maoni yao ambapo Escodee “jiwekee mipaka ya matumizi ya mitandao…, itakusaidia sana kutuacha sisi tunaokuheshimu tuendelee kukuheshimu…,usiichukulie mitandao kama ndio maisha yako yote baada ya kuwa nue ya uwaziri.”
“Wala usichukue kama ndio sehemu ya kusemea kushtakia kujitetea nk. Ukiwa makini utanielewa na utajitathimini wakati una matumizi madogo na mitandao na sasa hivi ni wakati gani heshima yako inashuka zaidi. Ukibaki kimya na kuacha CV zako zifanye kazi inasaidia kutozoeleka na kuonekana mapungufu yako mengine…,chunguza tena mwenendo wako juu ya matumizi ya mitandao. Nakuelewa sana na sio mmoja wa wapendao jina lako linapoelekea.”
Miss geeofficial aliandika, “tuache kidogo tutafakari kwanza ya CAG.”
Idrissultan aliandika , “Alaaaaa” huku Mjukuuwanombo akisema “Ntu ya dili.”
Muzzamilaccessories alisema, “kimeumana sie yetu macho tu,” na kuungwa mkono na Binmadiba aliyesema, “bado nawaza kwanini mzee alikuondoa kwenye wizara pindi yupo hai kwani nahisi kuna ukweli ndani yake hata wewe unaujua kwa Mungu si kwa mzungu Bro jisikilize mwenyewe tu kwa sauti yako ya ndani.”