Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa amelazimika kuitembelea familia ya Seleman Mpange, mkazi wa Kijiji cha Lukulunge Kata ya Mvuha Mkoani humo baada ya Familia hiyo ya Watu 8 kuzua taharuki kwa kutembea wakiwa hawana nguo (kama walivyozaliwa) asubuhi kutoka kijiji kimoja hadi kingine huku chanzo kikitajwa kuwa ni imani za kishirikina.
Katika hali isiyo ya kawaida Watu wanane wa Familia moja wakiwemo Watoto, Wakwe pamoja na Baba na Mama wa Familia hiyo walivua nguo zote na kutembea umbali wa zaidi ya kilometa tatu asubuhi, Aprili 7 mwaka huu wakidai wanatekeleza masharti ya mizimu.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya, Baba wa Familia hiyo, Seleman Mpange amesema ameamua kufanya hivyo ili kutii masuala ya mizimu, mila na desturi za ukoo wao, Mwenyekiti wa kijiji Kibwana Senza amesema Kuwa baada ya kupata taarifa za tukio hilo alitoa taarifa Polisi na kwamba tukio kama hilo hailijawah kutokea katika kijiji hicho.
Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa amesema msimamo wa Serikali ni kuwa suala hilo linatakiwa kuzungumzwa Kifamilia ili kubaini ukweli wa jambo hilo wakiwashirikisha Wazee wa kimila.