KUFUATIA changamoto iliyokuwepo ya bei kubwa ya vifurushi vya mitandao ya simu na kupelekea Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile kuahidi maboresho kufikia Aprili 2, 2021, kanuni mpya za vifurushi vya simu zimeanza kufanya kazi leo Aprili 2, 2021.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Global Publishers umebaini kuwa, badala ya kupungua, gharama za mabando zimepanda zaidi kuliko ilivyokuwa awali na kuzua sintofahamu kwa watumiaji wa mitandao hiyo.
Aidha, kupitia mitandao ya kijamii wananchi wakiilalamikia mitandao hiyo kwa kufanya kinyume na matarajio ya wananchi wengi walivyokuwa wakitegemea hasa kutokana na maagizo ya Waziri mwenye dhamana hiyo.
Hata hivyo mpaka sasa, si waziri, wala Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ama wamiliki wa mitandao hiyo ya simu ambaye amefafanua kwa wananchi kuhusu kwa nini gharama hizo zimepanda mara dufu. Tunaendelea kuwatafuta wahusika wenye dhamana ya mawasiliano ili kupata ufafanuzi na kuondoa sintofahamu kwa wananchi.