Gomes Avuruga Dili la Manula Al Merrikh

 


KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes ameibuka na kutamka kuwa kamwe hatakubali kumuachia kipa wake namba moja Aishi Manula aondoke katika kikosi chake kutokana na ubora wake alionao.


 


Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika juzi saa kumi jioni kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena, Bunju nje kidogo ya Dar es Salaam katika kujiandaa na mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita.


 


Hiyo ni baada ya kupata taarifa za kipa huyo kuwaniwa na Al Merrikh ya nchini Sudan ambayo nayo inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu huu.Akizungumza na Championi Jumatano, Gomes alisema kuwa amezisikia taarifa za kipa wake kuhitajika na Merrikh ambazo kwake hazimtishi akiamini Manula hatakwenda huko na badala yake ataendelea kubakia kukipiga Simba.




Gomes alisema kuwa ni ngumu kwake kumuachia Manula kwa hivi sasa kutokana na uimara, kiwango bora alichonacho hivyo atahakikisha anapambana kuishawishi Bodi ya Wakurugenzi ya Simba iliyo chini ya mwenyekiti wake Mohammed Dewji ‘Mo’ imbakize Simba.


 


Mfaransa huyo anapata jeuri ya kipa huyo kubakia Simba kutokana na timu hiyo aliyokuwa anaifundisha kutokuwa na uwezo wa kifedha kumsajili baada ya kuyumba kiuchumi.


 


“Mimi nilikuwepo Merrikh kabla ya kuja Simba, hivyo ninaifahamu vizuri timu hiyo akiwemo rais wake hivyo ni ngumu kumsajili Manula.


 


“Timu hiyo ninafahamu imeyumba kiuchumi hivi sasa hivyo hawana fedha ya kumsajili na kingine hata kama wangekuwa na fedha kiasi gani nisingeweza kumruhusu kuondoka Simba na hiyo ni kutokana na ubora wake.


 


“Siyo Merrikh hata klabu nyingine yoyote asingeondoka, lipo wazi Manula yupo katika kiwango bora zaidi, ni kipa anayejua majukumu yake vizuri.“Nimepata taraifa za kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo nitazungumza na viongozi kwa ajili ya kumuongezea mkataba mpya ili aendelee kubakia hapa Simba,” alisema Gomes.


STORI: WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA, Dar

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad