KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amefunguka kuwa kama kuna timu ina ndoto ya kushinda taji la Ligi Kuu Bara msimu huu, basi wasahau kuhusu hilo kwani kikosi chake kitafanya kila jitihada kuhakikisha wanatetea ubingwa huo mapema tu.
Simba imeshatwaa taji la ligi mara tatu mfululizo na msimu huu wameonekana kupata upinzani mkubwa kutoka kwa watani zao Yanga ambao wametangaza nia ya wazi ya kumaliza utawala huo wa misimu mitatu wa Simba.
Mpaka sasa Yanga ndiyo vinara wa msimamo wa Ligi Kuu na pointi zao 51 walizokusanya katika michezo 24 waliyocheza, Simba wao wanakamatia nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kupata pointi 49 kwenye michezo 21 waliyocheza.
Hii ina maana kama Simba watashinda michezo yao mitatu ya viporo iliyosalia wataishusha Yanga kwenye msimamo na kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi saba.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Gomes alisema: “Najua hakuna timu ambayo inashiriki ligi bila kuwa na malengo yao binafsi, na kuna baadhi ya wapinzani wetu ambao wamejipanga kutuvua ubingwa msimu huu.
“Lakini nikuhakikishie kuwa, tumejipanga kutumia faida ya michezo yetu ya viporo kuongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi saba, na ikiwezekana kutangaza ubingwa mapema.“Hii ni kwa sababu tunataka kujihakikishia nafasi ya kucheza tena michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.”
Stori na JOEL THOMAS, Dar es Salaam