Muda mchache baada ya kumalizika kwa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wananchi, wasomi, wanasiasa wampongeza huku wakisema imejaa matumaini kuelekea Tanzania mpya.
Rais Samia ametoa hutuba hiyo leo Jumanne Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao wa wizara mbalimbali aliowateua Aprili 4, 2021 baada ya kufanya mabadiliko.
Katika hotuba yake alizungumzia mambo mbalimbali huku akitoa maagizo ya kitu gani cha kufanya kwa kila wizara na vitu gani vya kuondoa.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Paul Luisulie ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) amesema hotuba ya Rais Samia inadhihirisha matamanio makubwa aliyonayo ya kutaka kuleta mabadiliko katika maendeleo ya Tanzania.
Amesema Rais anatamani kuleta mabadiliko kwa kutumia aina yake ya kipekee ya uongozi tofauti na mtangulizi wake ambaye pia alikuwa na aina yake ndiyo maana amejaribu kuwapa utaratibu kila wizara baada ya kuapishwa ili wajue nini wafanye.
“Anaonyesha kuwa kuna vitu alikuwa anakerwa navyo ambavyo alipokuwa Makamu wa Rais, baadhi ya vilivyokuwa havimpendezi ni matumizi ya mabavu katika kukusanya kodi, kufungia vyombo vya habari, ndiyo maana hata ametaka vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa vifunguliwe,” amesema Dk Luisulie.