Rais wa Iran ameamuru uchunguzi juu ya kile alichokitaja kuwa ‘’njama’’ ya kuvujishwa kwa kanda ya sauti ambapo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran alisema jeshi lina ushawishi zaidi kwenye masuala ya diplomasia.
Msemaji wa serikali Ali Rabiei ametangaza hayo leo, akiongeza kwamba rais ametaka uchunguzi ubaini ni nani alivujisha kanda hiyo yenye urafu wa masaa matatu ikiwa na mazungumzo kati ya mwanadiplomasia wake mkuu Javad Zarif na afisa mwengine wa serikali yake.
Kanda hiyo ambayo imevujishwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Juni, imetawala mijadala ya umma katika jamhuri hiyo ya Kiislamu, tangu vyombo vya habari vya kimataifa vilipoitangaza siku ya Jumapili.
Ali Rabiei amewaambia waandishi wa habari kwamba wanaamini uvujishaji wa kanda hiyo ni njama dhidi ya serikali, mfumo wake na maadili ya taasisi za ndani na pia dhidi ya masilahi yao ya kitaifa.