Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, ameshauri kuwapo kwa haja ya kutafakari upya jinsi ya kuurejea mchakato wa Katiba mpya utakapofufuliwa.
Hata hivyo, alisema kwa sasa ni bora kuiacha kwanza Serikali itulie kabla ya kuanza kuujadili mchakato huo.
Kauli ya Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, imekuja wakati joto la madai ya mabadiliko ya Katiba likianza kupanda upya baada ya mchakato huo kufifia tangu mwaka 2014 baada ya kupitishwa kwa Katiba inayopendekezwa.
Akizungumza juzi wakati wa kuwaapisha mawaziri 16 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alisema amejikuta akilitajataja Bunge la Katiba, kutokana na kusukumwa na watu kuhusu kufufua mchakato huo.
“Hivi nina maradhi gani na Katiba? Nadhani wamenisukuma sukuma sana; katiba katiba, lakini wasahau kidogo,” alisema Rais Samia juzi.
Alipoulizwa kwa simu jana, Jaji Joseph Warioba alisema: “Ngoja kwanza tuone intention (nia) ya Serikali. Katika mazingira haya uone nia ya Serikali tujue tuta revisit (tutarejea) wapi.
Kwa sababu utaratibu ule haukukamilika na muda umepita, kwa hiyo tukianza itabidi tukubaliane juu ya utaratibu.
Kwa sasa tuache kwanza Serikali itulie, tuone itapofika ndiyo tuanze kuzungumza.’’
Wadau wengine
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Chacha Wangwe aliandika katika ukurasa wake wa Facebook akionyesha imani ya mabadiliko hayo.
“Ni imani yetu tutapata Katiba mpya ndani ya uongozi wa Mama Samia. Kazi yetu itakuwa ni ku-push (kusukuma) bila kuchoka, maana katiba ni ajenda ya wananchi. Tunaamini sio rahisi kuingia na kuanza na mchakato na huenda ikawa ndio tafsiri ya maneno ‘wasahau kidogo.’ Tunakuombea hekima zaidi ili uone umuhimu wa sauti hizi.”
Alipoulizwa kwa simu jana, Bob Wangwe alisema endapo mchakato huo utaruhusiwa, kuna haja ya kutumia rasimu ya pili ya katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Katiba inayopendekezwa ili kupata mwafaka.
Pia, Wangwe alishauri kuundwa kwa timu ya wataalamu wa Katiba ili watoe mwongozo wa kufikia mabadiliko hayo.
“Kinachotakiwa kwa sasa ni utashi na utayari wa kufikia kwenye mabadiliko ya Katiba kwa sababu tumepata Rais mwenye utayari. Hii ni Katiba ya wananchi sio matakwa ya wanasiasa peke yao,” alisema.
Suala la kuundwa kwa kamati ya wataalamu wa Katiba pia limeungwa mkono na Deus Kibamba ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa, aliyesema kamati hiyo ndiyo itakayomshauri Rais mahali pa kuanzia na kuelekea.
“Kabla ya kuundwa kwa kamati hiyo, Serikali ipeleke muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatakayoanzisha kamati hiyo pamoja na marekebisho mengine,” alisema.
Kibamba alisema kama mchakato huo utaanzishwa, unapaswa kuanzia kwenye rasimu ya pili ya mabadiliko ya Katiba maarufu kama ‘Rasimu ya Warioba.’
“Mpaka kwenye rasimu hiyo hakukuwa na mgogoro. Tatizo lilianza wakati wa uwasilishaji wa rasimu hiyo bungeni, ambapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alizindua Bunge la Katiba, kabla rasimu haijawasilishwa, pale ilimaanisha rasimu haiko rasmi,” alisema.
Pia, Kibamba alisema kosa jingine lililofanyika ni kuivunja iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kabla hata mchakato haujakamilika.
“Tume ile ilitakiwa kuwa sekretarieti ya kushauri mchakato mpaka mwisho,” alisema.
Alisema kuwa Sheria ya Mabadiliko ilikuwa na upungufu, kwani ilishindwa kueleza njia za kutatua migogoro ikitokea, likiwamo suala la kuvunjwa kwa Tume na endapo ungetokea mgogoro upande mmoja wa Muungano.