Waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba amewaonya wanaotumia mtandao wa kijamii wa Twitter na kujifanya yeye akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya nchini Tanzania akibainisha kuwa wanamlisha maneno ambayo si yake.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 6, 2021 mwenyekiti huyo wa iliyokuwa tume ya mabadiliko ya katiba amesema, “sina akaunti katika mtandao wowote ule wa kijamii. Wanaofanya hivyo wanafanya kosa sana kutumia jina langu.”
“Wanaeleza mambo ambayo sijayasema, wananilisha maneno hawa nadhani hili halisaidii Taifa. Kuzungumza ninaweza lakini sio kuelezwa kuwa nimesema kitu fulani wakati sijasema.”
Katika mtandao huo mtu anayejiita Joseph Sinde Warioba ameandika, “nimemsikiliza mheshimiwa Rais Samia hotuba yake imejaa matumaini, upendo na ni shirikishi,. Nitatafuta mihadi naye tufanye mazungumzo juu ya Katiba Mpya. Katiba Mpya ni msingi wa umoja, utu, haki, amani, udugu na mshikamano kwenye Taifa letu.”
Katika akaunti hiyo ambayo Jaji Warioba amesema si yake inaonyesha kuwa imefunguliwa Aprili, 2021 na anayeitumia ameandika masuala mbalimbali kuhusu mchakato wa katiba.