Baraza la utawala wa kijeshi nchini Chad limekataa ombi la mazungumzo ya kusitisha vita na waasi ambao imekuwa ikipigana nao tangu kifo ambacho hakikutarajiwa cha rais Idris Deby. Baraza hilo la kijeshi lilichukua mamlaka mapema wiki hii baada ya bwana Deby kuuawa wakati wa vita na waasi.
Likiongozwa na mtoto wa Deby, baraza hilo lilisema litasimamia serikali ya mpito itakayohudumu kwa miezi 18 kabla ya kuitisha uchaguzi. Viongozi wa upinzani na waasi wameshutumu hatua ya jeshi kuchukua madaraka kama mapinduzi.
Bwana Deby aliyekuwa na umri wa miaka 68 alikuwa ameshinda uchaguzi wa urais wakati jeshi lilipotangaza siku ya Jumapili kwamba alikuwa ameuawa katika vita dhidi ya waasi katika eneo la kaskazini mwa jimbo la Kanem katika taifa hilo la katikati mwa Afrika.
Waasi hao wanaojulikana kwa jina Front for Change and Concord in Chad (FACT),walifagia eneo la kaskazini siku ya uchaguzi wakitaka bwana Deby kusitisha uongozi wake wa miaka 30.
Siku ya Jumamosi, waasi walisema kwamba wako tayari kukubaliana kisiasa lakini hawaungi mkono mapinduzi hayo yaliomuweka madarakani mtoto wa Deby Jenerali Mahamat Deby.
Lakini siku moja baadaye , baraza la kijeshi lilisema kwamba halitajadiliana na waasi ambao ilikuwa ikipigana nao.
”Tukikabiliwa na hali ambayo inahatarisha taifa la Chad na udhabiti wa eneo zima sio wakati wa mazungumzo na watu wasiofuata sharia”, msemaji wa baraza hilo la kijeshi Azem Bermendao Agouna alisema katika taarifa.
”Ni waasi ndio sababu tunawapiga mabomu, tunapigana nao, ni hiyo tu”.
Agouna alisema kwamba baadhi ya wasi walitoroka katika nchi jirani ya Niger. Alitoa wito kwa mamlaka nchini humo kusaidia kuwakamata na kuwaleta mbele ya haki wahalifu hao wa kivita.
Alisema kwamba kiongozi wa FACT, Mahamat Mahadi Ali alikuwa anasakwa kwa uhalifu wa kivita nchini Libya ambapo kundi lake la waasi linapigana.
Kundi hilo liliundwa mwaka 2016 likiwa na lengo la kupindua serikali ya Chad na limehusishwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Mahamat Idriss Deby , mwana wa rais Idriss Deby wakihudhuria mazishi yake.
Baraza la Kijeshi lipo katika shinikizo kali kutoa mamlaka kwa serikali ya mpito inayoongozwa na raia haraka iwezekanavyo.
Baraza la Umoja wa Afrika kuhusu amani na usalama liliwasilisha wasiwasi wake kuhusu unyakuzi huo wa mamlaka uliotekelezwa na jeshi huku Ufaransa na mataifa jirani yakipigania kuwepo kwa suluhu itakayoafikiwa kati ya jeshi na raia.
Bwana Deby alizikwa siku ya Ijumaa katika mazishi ya kitaifa yaliohudhuriwa na rais Emmnuele Macron na maelfu ya raia wa Chad.
Afisa aliyepewa mafunzo, bwana Deby alichukua madaraka 1990 kupitia mapinduzi ya kijeshi. Alikuwa mwandani wa karibu wa Ufaransa na mataifa ya Magharibi katika vita dhidi ya Jihad katika eneo la Sahel barani Afrika.