Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un amesihi raia wa taifa lake kujitayarisha na janga kubwa linalowadia, kufuatia makundi ya haki za kibinadamu kuonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kuzorota kwa kiuchumi.
Akizungumza katika mkutano, Bwana Kim alionekana kulinganisha hali ilivyo sasa hivi na janga kubwa la njaa lililotokea miaka ya 1990.
Korea Kaskazini imefunga mipaka yake kwasababu ya janga la virusi vya corona.
Pia, imesitisha uhusiano wake wa kibiashara na China hatua iliyokwamisha uchumi wake.
Aidha, imewekewa vikwazo vya kiuchumi kimataifa kwasababu ya mpango wake wa nyuklia.
Katika hali isiyo ya kawaida ya yeye kukubali kwamba nchi inapitia changamoto haswa, kiogozi huyo, aliwataka maafisa wa chama kukabiliana na "kipindi kigumu' angalau nchi iweze kuepushia wananchi wake zahama hiyo hata ingawa kidogo tu".
Alitumia neno maarufu kwa maafisa wa Korea Kaskazini wanapozungumzia changamoto ya nchi wakati wa kiangazi kikali miaka ya 1990, pale Muungano wa Usovieti ulipoacha Korea Kaskazini bila usaidizi wa msingi. Takriban watu milioni 3 inasemekana kuwa walifariki dunia kipindi hicho.
"Sio kawaida kwa kiongozi Kim Jong-un kuzungumzia changamoto anazopitia lakini anaonekana kuchukua muelekeo mpya," Colin Zwirko, mchambuzi wa Korea Kaskazini wa NK News, amezungumza na BBC.
"Kwa mfano Oktoba mwaka jana, alitoa hotuba na kusema kwamba yeye mwenyewe ameshindwa kuleta mabadiliko yaliyokusudiwa."
Mapema wiki hii, Bwana Kim alionya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na "hali mbaya zaidi kuwahi kutokea" na "kutabiri changamoto kadhaa".
Hali ni mbaya kiasi gani?
Kumekuwa na onyo kwa miezi kadhaa kwamba Korea Kaskazini inapitia changamoto chungu nzima.
Taarifa za janga hilo zinaonekana kujitokeza katika miji iliyo karibu na mpaka wa China, ambako magendo hufanyika.
Bei ya mahidi, chakula kinachopendwa na wengi vijijini Korea Kaskazini, inasemekana kuwa imepanda vibaya na wakati mwingine bei yake ni zaidi ya mshahara wa mtu wa mwezi.
Lina Yoon, mtafiti kutoka Shirika la Human Rights Watch, amesema katika ripoti ya hivi karibuni, akirejelea vyanzo ambavyo hakuvitaja nchini humo, kuwa "hakuna chakula chochote kinachoingia Korea Kaskazini kutoka China kwa takriban miwezi miwili sasa".
"Kuna wengi wanao omba omba mtaani, wengine wanafikiri dunia kutokana na baa la njaa katika maeneo ya mpakani, hawana sabuni, dawa za kupiga mswaki wala betri."
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu Korea kaskazini, Tomás Ojea Quintana, alionya mwezi uliopita katika taarifa iliyoangazia "uhaba mkubwa wa chakula" ambako tayari kumesababisha utapiamlo na njaa.
"Kumeripotiwa vifo ambavyo chanzo chake ni njaa, na idadi ya vifo hivyo imeongezeka zaidi kwa watoto na watu wazima ambao wamegeukia kuwa omba omba kwasababu familia zimeshindwa kukimu mahitaji yake."
Bado haijafahamika ikiwa kuna msaada wowote unaoingia nchini humo kwa sasa.
Ikiwa ni nchi yenye kudhibitiwa kikamilifu na serikali, uchumi wa Korea Kaskazini ni miongoni mwa iliyo huru zaidi duniani na inasemekama hauna tija kwa raia wake.
Gharama kubwa ya kuendeleza jeshi nchini humo na mifumo ya usalama imefanya raia wa kawaida kuumia zaidi.
Vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa kushinikiza Korea kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia kumefanya hali kuzorota zaidi pamoja na kufunga mipaka yake kama njia ya kukabiliana na virusi vya corona.
Biashara na China imekwama tangu mapema 2020, na kusitisha usambazaji wa bidhaa muhimu kwa maafisa na raia wake.
Na pia kuna dalili zinazoashiria kuwa Pyongyang inapata shinikizo ya kufungua tena mipaka yake, Bwana Zwirko amesema.
"Korea Kaskazini imeonesha dalili za kutaka kuongeza shughuli za kibiashara na China tena. Wamepitisha sheria mieiz michache iliyopita kusaidia kufufua tena biashara ya mpakani.
Hadi kufikia sasa, Korea kaskazini inadai kuwa kufunga mipaka yake kumefanya waepuke ugonjwa wa virusi vya corona, ingawa wachambuzi wanatilia mashaka dai hili.