Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya kutokuwepo tena kwa kimbunga ‘Jobo’ ambacho kilitabiriwa kupiga nchini katika baadhi ya maeneo ikiwemo Dar es Salaam hii leo tarehe 25/04/2021.
“Taarifa hii inahuisha taarifa ya kimbunga hafifu “Jobo” iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) jana mchana tarehe 24/04/2021. Mwenendo wa kimbunga hafifu “Jobo” unaonesha kuwa katika kipindi cha saa sita zilizopita “Jobo” imepoteza nguvu yake wakati kikiingia nchi kavu kusini mwa mkoa wa Pwani na Dar Es Salaam usiku wa tarehe 24/04/2021. Hali hii ilisababishwa na kuendelea kuimarika kwa upepo kinzani katika mwelekeo wa kimbunga hicho.
Aidha, mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yamesambaa baharini karibu na maeneo ya kusini mwa pwani ya Tanzania na Msumbiji.
Hivyo kwa sasa, kimbunga hafifu “Jobo” hakipo katika nchi yetu na hakuna madhara ya moja kwa moja yanayotarajiwa. Hata hivyo masalia ya mawingu yanayoambatana na kilichokuwa kimbunga “Jobo” yanaweza kusababisha mvua katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika.