Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini TMA imesema Kimbunga JOBO kimepunguza kasi mara baada ya kuingia kwenye mazingira ya upepo kinzani hivyo kwasasa kimbunga hicho ni hafifu.
TMA imetoa taarifa hiyo leo April 24, ikielezea mwenendo wa kimbunga “Jobo” kilichopo bahari ya Hindi ambacho kipo umbali wa kilomita 200 mashariki mwa kisiwa cha Mafia nakusewa kuwa kimbunga hicho kimekuwa hafifu kinachosafiri kwa kasi ya kilometa 18 kwa saa baharini.
TMA imesema kimbunga hicho hafifu kinatarjia kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika maeneo machache hususan ya ukanda wa Pwani kadri kinavyosogea nchi kavu kwa siku ya leo tarehe 24 na kesho 25 mwezi Aprili, 2021 na kusababisha mawimbi makubwa.
Pia Mamlaka hiyo imesema maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja.
Aidha wananchi wameshauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka hiyo pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.