KIMENUKA! Unaweza kusema hivyo baada ya kigogo mmoja kwenye kamati ya ufundi Yanga kudai kuwa baadhi ya wajumbe wamekuwa hawashirikishwi kwenye mambo ya usajili.
Inadaiwa kuwa, inaweza kuwa moja ya sababu ambazo zinaifanya Yanga ikwame kutakata kwenye michezo yake hasa raundi hii ya pili ya Ligi Kuu Bara, hiyo ni kutokana na kutokuwepo kwa ushirikiano kwenye usajili kati ya mabosi wa timu hiyo na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ambayo inaundwa na wachezaji wa zamani.
Msimu huu, Yanga imekuwa na sehemu kubwa ya wachezaji wengi wapya ambao waliwasajili dirisha kubwa wakiwemo Michael Sarpong, Carlinhos, Tuisila Kisinda, Mukoko Tonombe na wengineo huku dirisha dogo wakiwaongeza wa kimataifa Fiston na Said Ntibazonkiza ‘Saido’.
Yanga ilianza ligi vizuri lakini huku wakicheza michezo 21 bila kufungwa lakini hivi karibuni imekuwa na mwenendo wa kusuasua licha ya kuwa inaongoza ligi ikiwa na alama 51 na katika mechi saba zilizopita imeshinda mara moja, sare tano na kupoteza moja.
Mjumbe wa Kamati ya Ufundi wa Yanga ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji nyota wa timu hiyo miaka ya nyuma, Sekilojo Chambua, ameliambiaChampioni Jumamosi kuwa, huwa hawashirikishwi kwenye masuala ya usajili wa wachezaji na msimu huu GSM ndiyo ambao walikuwa wanafanya kazi hiyo ya kushusha majembe.
Chambua alisema huwa hawashirikishwi sana kwenye masuala ya usajili licha ya kuwa yupo kwenye kamati ya ufundi na hilo hupelekea kuwa na matatizo ndani ya timu kwa sababu viongozi hawafikirii nani anaweza akatumika kwenye ‘scouting’ ya kujua ni mchezaji gani atawafaa kwa wakati uliopo na baadhi ya wachezaji waliosajiliwa hawatoshi kuwa sehemu ya klabu hiyo kubwa na inayopendwa na mashabiki wake.
“Nipo kwenye Kamati ya Ufundi, lakini hatujawahi kusajili hata mchezaji mmoja, wachezaji huwa wanasajili viongozi na wafadhili wetu GSM, hiyo ndiyo sababu ambayo inapelekea matatizo ndani ya timu, kwa kuwa wanashindwa kututumia kwenye scouting ya kujua mchezaji gani mzuri na atafaa na hata ukiwatazama wachezaji waliopo sasa wengi hawatoshi,” alisema Chambua.