Kwa nini LG imeamua kuacha kutengeneza simu






LG mtengenezaji mkubwa wa tatu wa simu za mkononi ulimwenguni tangu mwaka 2013 hadi miaka ya hivi karibuni na imejitahidi kutengeza simu za mkononi katika mazingira ya ushindani mkali ya soko ambalo linajumuisha Apple, Motorola au Huawei.


Changamoto hizo ziliifanya kampuni hiyo siku ya Jumatatu kutangaza hatua ya kufunga biashara ya kutengeza simu za rununu kote duniani.



Kuanzia mapema mwezi Januari kampuni hiyo kubwa ya elektroniki ya Korea Kusini ilisema inatafakari mbinu zote zitakazoisadia kukomesha hasara baada ya kuandikisha karibu miaka sita hasara inayokadiriwa kuwa karibu dola bilioni 4.5.



Hatua ya kufunga kitengo cha utengenezaji simu itakuwa na athari katika maeneo yote yaliyo na matawi yake. Hasa Amerika kusini, ambayo ni ya tatu katika uuzaji wa bidhaa.



Kufikia mwezi Juni mwaka 2020, LG ilikuwa inashikilia asilimia 4.5 ya soko katika eneo hilo, ikilinganishwa asilimia 42.5 ya Samsung.



"Uamuzi wa LG kujiondoa katika biashara ya utengenezaji simu simu za rununu iliyo na ushindani mkali itawezesha kampuni hiyo kuelekeza rasilimali zake katika ukuaji wa aina nyingine kama vile vifaa vya gari la umeme, vifaa vya kuunganisha bidhaa za umeme, nyumba nzuri, roboti, akili ya bandia na kadhalika, "kampuni hiyo ilisema katika taarifa yake.



Lakini licha ya hasara, kampuni ya ushauri ya Counterpoint inaelezea kufungwa huko ni kutokana na ukweli kwamba "wakati enzi za simu za rununu zilipoanza, LG ilipitisha mfumo wa uendeshaji wa Microsoft badala ya Android na ikachukua muda kuingia kwenye mfumo wa uendeshaji wa Google."



Kwa mujibu wataalamu, hiyo huenda ilikuwa kigezo ambacho kilichangia simu zao kupoteza umaarufu.



"Licha ya kuzindua bidhaa za teknolojia ya kisasa, LG ilishindwa kuwaridhisha wateja, hali ambayo iliwafanya kubadili mbinu ya utendakazi wao," anasema mshauri wa masuala ya kiteknolojia.



Kando na hilo lazima tuongeze kwamba LG iliamua kujiingiza katika ushindani wa kutengeza simu za rununu za hali ya juu na za wastani ambazo zinatengenezwa na kampuni zingine ambazo zilikuwa na ''ubunifu zaidi''.



Kwanza ifahamike kwamba hatua ya kufunga kwa kitengo cha utengenezaji simu cha LG haimaanishi simu za kampuni hiyo zitaacha kufanya kazi ndani ya usiku mmoja.



Kampuni hiyo imethibitisha kwamba katika miezi ijayo itatoa usaidizi kwa wale walio na simu za kampuni hiyo maarufu ya Korea Kusini inayofahamika kwa utengenizaji televisheni zake na bidhaa nyingine za elektroniki.



Biashara ya simu ni ya chini zaidi katika vitengo vitano vya LG na inachangia asilimia 7.4 ya kipato.



Hivi sasa, sehemu yake ya soko la simu ya rununu ni karibu 2%.



LG bado ina wateja wengi katika biashara ya elektroniki, hasa vifaa vya nyumbani na televisheni.



Ni ya pili katika uuzaji wa Televisheni duniani baada ya Samsung.



Mwezi Disemba mwaka jana ilizindua ubia na kampuni ya kimataifa ya Magna ili kutengeneza vifaa muhimu vya magari ya umeme.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad