Kwanini ni vigumu kukabiliana na kundi la IS Msumbiji?






Shambulizi la hivi karibuni lililosababisha wengi kupoteza maisha kutokana na shambulizi lililotekelezwa na wapiganaji wa jihadi wa kundi la Islamic State kaskazini mwa Msumbiji limeshutua dunia.


Mamia ya wapiganaji waliokuwa wamejihami walifanikiwa kudhibiti mji ulio karibu na mradi kubwa zaidi wa gesi Afrika. Waliwaua makumi ya watu, wenyeji na wataalamu huku wakiacha miili iliyokatwa vichwa mitaani.



Lakini je hili lilitokea vipi, kwanini serikali ya Msumbiji imeshindwa kukabiliana na wanamgambo na je nini kinahitajika kushinda vita hivi?



Wanamgambo ni kina nani?

Wanajiita al-Shabab, neno la kiarabu linalo maanisha "vijana wadogo" .

Hii inapotosha kwasababu wao sio kundi moja na lile linalohusishwa na kundi la al Qaeda nchini Somalia ambao pia wanajulikana kwa jina hilo.



Badala yake kundi hili liliahidi kutii kundi pinzani la IS mwaka 2019 ambalo lina makao yake nchini Iraq na Syria.



Wamechukua jina la Islamic State Central Africa Province (ISCAP) ambalo pia nalo linapotosha kwa sababu Msumbiji sio sehemu ya Afrika ya Kati.



Katika kile ambacho kinaonekana kujirejelea kwengineko duniani, kama vile Mali, Iraq na Nigeria, kundi hili la wanamgambo limetokana na malalamishi ya wenyeji ambao wanahisi kutengwa na kubaguliwa na serikali yake yenyewe.



Mkoa wa Cabo Delgado uliopo Msumbiji ambako kundi hilo linaendesha shughuli zake, ni zaidi ya kilomita 1,600 kutoka mji wa Maputo lakini kuna mradi mkubwa unaoendelea eneo hilo wa gesi asili.



Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Ufaransa ya Total na unakadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 60 za Marekani ukiwa na uwekezaji kutoka nchi za Uingereza.



Wenyeji wanalalamika kuwa hawajafaidika na mradi huo na kusababisha kuanza kwa kundi hilo la wanamgambo mwaka 2017, na baadaye likawa la kimataifa baada ya kuungwa mkono na kundi la IS.



Kilichotokea wikendi iliyopita katika mji wa Palma, kundi la jihadi lilifanya mashambulizi kwa kutumia silaha kama vile bunduki, roketi na hata grunedi.



Kulingana na video zilizowekwa na kundi la IS mtandaoni, wanamgambo wote walionekana kujifunga vitambaa vya rangi nyekundi kichwani.



"Hata kama ni wanamgambo wa eneo," amesema Olivier Guitta, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Jihadi Afrika, "al-Shabab imekuwa na uhusiano na wanamgambo wa Kiislamu Afrika Mashariki.



Viongozi wenye msimamo mkali wametoa usaidizi wa misingi ya kidini na hata mafunzo ya kijeshi kwa vijana wa Msumbiji kaskazini."



Kwa hiyo shambulizi hili ni la eneo ambalo limejificha ndani ya wanamgambo wa IS na kuvutia nadharia duniani kwa ghasia mbaya wanazotekeleza na pia kwa ukaribu wao na eneo lenye mradi mkubwa wa kibiashara.



Nini kifanyike kushinda kundi hili?

Hadi kufikia sasa juhudi kubwa zaidi zinahitajika.



Itambuliwe kwamba ni tatizo kubwa, serikali ya Msumbiji iliajiri zaidi ya wanajeshi 200 "washauri" kutoka kwa kampuni binafsi ya kijeshi nchini Urusi, kwa jina Wagner, Septemba 2020.



Hawa wengi wao ni wanajeshi waliokuwa wakihudumu katika kikosi maalum nchini Urusi ambao pia wamekuwepo katika nchi kama vile Syria, Libya na kwengineko.



Waliingia nchini Msumbiji wakiwa na ndege zisizokuwa na rubani na data zao walizokuwa wamezichambua lakini mchambuzi Olivier Gitta anasema kuwa mambo hayakwenda vile walivyokuwa wanatarajia.



"Baada ya kufanyika kwa mashambulizi kadhaa na vifo pia kuripotiwa katika eneo lenye msitu mkubwa la Cabo Delgado, Kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi imerejea tena kupanga upya mkakati wao."



Tatizo la hivi karibuni zaidi likiwa udhaifu wa vikosi vya usalama vya Msumbiji na pengine tofauti za wanasiasa.



Brigedia Ben Barry kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kimkakati amesema kundi la IS limedhihirisha uwezo wake wa kupigana katika maeneo yenye majengo na hilo limejitokeza kuwa changamoto kwa Msumbiji na washirika wake.



"Ili mfanikiwe katika vita vya mjini kunahitaji serikali kuwa na uongozi wa hali ya juu na mafunzo ya kutosha yanayojumuisha mbinu za kukabiliana mijini. Na hili linaweza kuelezea udhaifu wa vikosi vya Msumbiji. Wanaonekana kukosa uungwaji mkono kutoka kwa washauri wa nchi za Magharibi na pia uwezo mdogo wa kutumia nguvu ya anga, silaha za kisasa na magari ya kivita vyote hivyo vilikuwa lazima katika kukabiliana na wanamgambo wa kundi la IS kutoka miji ya Iraq na Syria."



Siku za hivi karibuni, Marekani imepeleka wanajeshi wake kuimarisha jeshi la Msumbiji na pia Ureno, iliyotawala nchi hiyo wakati wa ukoloni, pia nayo imeahidi kupeleka jeshi lake dogo kutoa mafunzo.



Inasemekana Ufaransa inafuatilia hali ilivyo katika kisiwa cha karibu cha Mayotte na Afrika Kusini inafuatilia kwa karibu majirani zake.



Hata hivyo, kujihusisha kijeshi kwa nchi za Magharibi kutakuwa na hatari zake.



Pia aliongeza kuwa "jukumu la Afrika Kusini ambayo [wanajeshi wake walinusuru wengi waliokuwa wamenaswa katika shambulio la hivi karibuni] kama mtekelezaji wa amani wa eneo huenda pia ikajumuishwa".



Mbinu zinazotumika na kundi la IS ni za kinyama na hatari sana. Tofauti na kundi la al-Qaeda ambalo pia linatekeleza vitendo vya kutisha, mara nyingi huwa linajitahidi kupata uungwaji mkono kutoka kwa wenyeji lakini wanamgambo hao wa Msumbiji wametekeleza shambulizi ya kuua wenyeji na hata kuwachinja vichwa.



Katika moja ya shambulizi mwaka huu hata kijana wa miaka 11 hakupona kuuawa mbele ya mama yake.



Kwa kipindi kifupi, matendo hayo yanasababisha hofu lakini pia ikumbukwe ni vigumu kwa kundi la wanamgambo kuendelea bila kukosa kuungwa mkono na wenyeji.



Kundi la Al-Qaeda nchini Iraq lilifanya makosa ya kushambulia wenyeji Waislamu Wakisunni katika eneo la Anbar mwaka 2007 - na kuanza adhabu kama vile kukata wanaume vidole kwa kuvuta sigara lakini muungano uliokuwa unaongozwa na Marekani ukafanikiwa kushawishi wenyeji kusimama dhidi ya kundi hilo na likawashinda.



Msumbiji inaweza ikachukua muda lakini mkondo ukawa huo.



Kukabiliana na wanamgambo sio tu suala la ushindi wa wanajeshi lakini pia inajumuisha kushawishi wenyeji na wakuamini "kifikra na mioyo yao yote".



Kwa hiyo kushinda wanamgambo, kwanza itahitaji kampeni nchini Msumbiji yenye kujumuisha utaratibu wa hali ya juu na vifaa stahiki pamoja na usaidizi kutoka nchi zingine.



Lakini pia ili ifanikiwe vita hivi, itahitajika juhudi zaidi ya hizi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad