Lipumba amshauri Samia kuweka malengo kupata tuzo ya Mo Ibrahim




Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kujiwekea malengo ya kutwaa tuzo ya Mo Ibrahim ya utawala bora kwa kurejesha utawala bora unaojali msingi ya demokrasia.


Ameyasema hayo leo Alhamisi Aprili mosi, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam akitaka pia mawaziri na watendaji wa Serikali wapewe mikataba ya kupimwa utendaji wao.



"Rais Samia ajiwekee lengo la kushinda tuzo ya Mo Ibrahim. Huyo ni tajiri aliyeanzisha taasisi ya kuzishawishi nchi za Afrika kuwa na utawala bora. Wanaangalia maraisi waliostaafu na waliotimiza vigezo vya utawala bora," amesema Profesa Lipumba.



Amesema wakati huu ambao Rais Samia yuko kwenye fungate la urais anapaswa kujipanga, kujijenga kisiasa badala ya kutafuta maslahi.



"Iwe ni miaka minne na nusu au tisa na nusu atakayotawala, basi ajiwekee lengo la kupata tuzo. Ajiwekee lengo la kulinda na kuheshimu haki za binadamu na utawala bora, ukifika muda watu waone kuwa anafaa kupata tuzo ya Mo Ibrahim," amesema.



Pia Profesa Lipumba amemtaka Rais Samia atambue kuwa uchaguzi mkuu wa 2020 haukuwa halali na hivyo aanze mkakati wa mabadiliko ya katiba yatakayoleta tume huru ya uchaguzi.



Ameendelea kusema kwakuwa Rais Samia alikuwepo kwenye Bunge la Katiba anajua mabadiliko hayo yanawezekana.



"Bahati nzuri amemteua Profesa Kabudi (Palamagamba) kuwa waziri wa katiba na sheria. Ni matumaini yetu kwamba tuwe na katiba yenye maoni ya wananchi.”



"Ndani ya rasimu ya Jaji Warioba, kuna mfumo wa tume huru ya uchaguzi. Makamishna waombe wafanyiwe tathmini, sheria ya uchaguzi ibadilishwe iendane na rasimu ya katiba ili tuwe na tume huru maana hii iliyopo ni tume ya kupanga matokeo," amesema.



Kwa upande mwingine, Profesa Lipumba amemshauri kiongozi mkuu huyo wa nchi  kuwapa mikataba ya utendaji mawaziri na watendaji wa serikali ili kupima utendaji wao na kuwawajibisha.



Huku akitoa mfano wa kukamatwa kwa aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko, Profesa Lipumba amesema Rais Samia ameonyesha uwajibikaji.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad