Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene ameagiza Jeshi la Polisi nchini kuwanyang’anya leseni madereva 10 wa mabasi yanayofanya safari zake katika Mikoa mbalimbali nchini kutokana na kufanya makosa yanayojirudiarudia.
Akizungumza jijini Dodoma leo Alhamisi Aprili mosi, 2021 Simbachawene amesema madereva watakaochukuliwa hatua leseni zao zitashikiliwa kwa kipindi cha miezi mitatu.
Amesema baada ya muda huo watatakiwa kufanya mtihani wa kuwapima katika kazi hiyo na wakifaulu watarudishiwa leseni kwa ajili ya kuendelea na kazi akibainisha kuwa wanakabiliwa na kosa la kuendesha mabasi kwa mwendo kasi.
Amewataja madereva hao na kampuni zao kwenye mabano kuwa ni Allan Msangi (Capricon), Hussein Dudu (Kimotco), Selemani Selemani (Al Saedy), Athuman Mnzava (BM Coach), Juma Simba (Baraka Classic) na Salum Salum (Maning Nice).
“Yupo Frank Masawe kampuni ya Machinga, Innocent Thomson kampuni ya Ester Luxur, Nassib Nassoro kampuni ya NBC Classic na Michael Mkindi kampuni ya Kilimanjaro Express,” amesema Simbachawene.
Simbachawene ameagiza polisi kupitia kikosi cha usalama barabara kuwapeleka mahakamani madereva hao.