MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kufuatilia majadiliano ya kuimaliza kesi iliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) dhidi ya mwenyekiti mtendaji wa PAP, Harbinder Seth na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Joseph Makandege.
Mahakama hiyo pia imeelekeza upande wa mashtaka kushughulikia shauri hilo kwa hekima na kuzingatia haki za binadamu pamoja na kufuatiliana kujua upelelezi umefikia hatua gani.
Hiyo ni baada ya siku 45 zilizotolewa na mahakama hiyo kwa washtakiwa hao kuisha bila kufanya majadiliano na DPP.
Februari 25, 2021 mahakama hiyo iliamuru majadiliano ya kukiri mashtaka yaliyowasilishwa kwa DPP dhidi ya Seth na Makandege, yasikilizwe ndani ya siku 30, kuanzia siku hiyo.
Aprili 8, 2021 mahakama hiyo iliongeza siku 15 ili washtakiwa hao kuendelea na majadiliano ya kukiri na mashtaka yao.
Uamuzi huo umetolewa jana Alhamisi Aprili 22, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya washtakiwa hao kupitia mawakili wao kuiomba mahakama hiyo iondoke mashtaka dhidi ya washtakiwa hao baada ya upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.