Jopo la Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) imempitisha Jaji Martha Koome kuwa Jaji Mkuu mpya wa Kenya na kuweka historia ya aina yake kwa Kenya na Bara la Afrika.
Jaji Martha Koome, wa Mahakama ya Rufaa, atakuwa Jaji Mkuu wa kwanza Mwanamke katika historia ya nchi hiyo na pia atakuwa wa 15 nchini humo na wa tatu chini ya Katiba mpya ya nchi hiyo, Jaji huyo atachukua hatamu kutoka kwa Jaji David Maraga aliyestaafu wadhifa huo.
Jina lake tayari limewasilishwa kwa rais Uhuru Kenyatta ili kuidhinishwa katika nafasi ilioachwa na Jaji mkuu mstaafu David Maraga.
Uteuzi wake unajiri saa chache tu baada ya mahakama kuu kutengua uamuzi wa mahakama ambao ulizuia Tume ya huduma za mahakama kutomtangaza mshindi wa shughuli iliokuwa ikiendelea ya kumtafuta jaji huyo kabla ya kesi hiyo kukamilika.
Pingamizi nne ziliwasilishwa mahakamani na kufanikiwa kusimamia shuguli ya tume hiyo iliokuwa ikiendelea, zikihoji kwamba watu wote 10 waliowasilisha maombi walikuwa hawajawasilisha stakhabadhi zao za kutangaza mali wanayomiliki kama inavyohitajika.
Lakini mahakama ya rufaa iliamuru kwamba Mahakama kuu haina uwezo wa kisikiliza suala hilo. Iwapo ataidhinishwa na rais , atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa jaji mkuu.
Lakini je Martha Koome ni nani haswa?
Jaji Martha Koome alizaliwa katika Kijiji cha Kithiu, katika kaunti ya Meru 1960. Jaji Koome baadaye alisomea shahada ya sheria katika Chuo kikuu cha Nairobi ambapo alifuzu 1986 na na kujiunga na chuo cha mafunzo ya Sheria nchini Kenya mwaka uliofuata.
Alianzisha Ofisi yake ya huduma za uanasheria 1988, na baadaye akajiunga na Huduma ya mahakama 2003 na kuhudumu katika mahakama tofauti kote nchini, wakati ambapo pia alihudumu kama mwanachama wa chama cha wanasheria nchini Kenya LSK.
Baadaye alijiunga na Chuo kikuu cha London ambapo alisomea shahada ya uzamili kuhusu sheria ambapo alifuzu na kupata cheti cha Sheria ya Umma ya kimataifa 2010.
Mwaka 2011 , alipandishwa cheo na kuwa jaji wa mahakama ya rufaa na mwezi Septemba mwaka huohuo, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Muungano wa Mahakimu na Majaji nchini Kenya. Jaji Koome , katika kipindi chake cha miongo mitatu amekuwa mtetezi wa haki za wanawake na ustawi wa Watoto.
Kuna wakati mmoja alihudumu kama mwenyekiti wa baraza la kitaifa la Jopo Maalum kuhusu usimamizi wa haki za watoto ambapo alisaidia katika kufanyia marekebisho sheria ya Watoto.
Hatua hiyo pamoja na nyenginezo kuhusu ustawi wa Watoto mwaka uliopita ilimsaidia kuwa nafasi ya pili miongoni mwa watu muhimu wa mwaka 2020 nchini Kenya taji linalotolewa na Umoja wa mtaifa.
Alinukuliwa akisema: Watoto hawana sauti , hivyobasi niliamua kuwazungumzia kwasababu natambua kwamba wao ni daraja la siku za usoni na iwapo hatutawalea vizuri , siku zetu zijazo zitakuwa hatarini. Natambua kwamba watoto wapo katika mazingira magumu kutokana na umri wao mdogo.
”Pia Natmbua iwapo wanazozana na sheria ama iwapo ni waathiriwa wa makosa, ni kutokana na kufeli kwa mfumo uliopo,’ alisema.
Jamii na familia zimeshindwa kulinda watoto. Jaji Koome ni mama wa watoto watatu.