KIONGOZI wa juu wa Shirika la Dawa nchini Denmark ameanguka na kupoteza fahamu wakati Serikali ikitangaza kusitisha kuwapa wananchi wake chanjo ya AstraZeneca, dhidi ya Covid-19 Jumatano, Aprili 14, 2021.
Kipande cha video na picha zilizosambaa mtaandaoni kinamwonyesha Bi. Tanja Erichsen, ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Dawa la Denmark, aliyekuwa amesimama mbele ya waandishi wa habari, alianguka ghafla chini na kupoteza fahamu wakati tangazo hilo la kusitisha chanjo likitolewa na mamlaka yake.
Wanaume watatu waliwahi kumnyanyua na kumpa huduma ya kwanza. Baadaye alikimbiza hospitali kwa ajili ya uchunguI na matibabu ambapo tayari ameshapata nafuu na kuruhusiwa.
Denmark ndiyo imekuwa nchi ya kwanza Barani Ulaya kusitisha kabisa matumizi ya chanjo ya AstraZeneca kwa maelezo kuwa inagandisha damu.
Kuna kesi mbili nchini humo, zimeripotiwa na kuthibitika za watu ambao walipewa chanjo ya AstraZeneca ambayo imesababisha damu zai kuganda. Miongoni mwao ni mwanamke mwenye umri wa miaka 60 ambaye baada ya hali hiyo kumtokea, hali yake ya afya ilibadilika na kuwa mbaya sana.