Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amesema Mkoa wa Shinyanga hauna tena mauaji ya vikongwe kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na vyombo vya vya ulinzi na usalama zilizofanikisha kuyakamata makundi ya mapanga yaliyokuwa yanatekeleza mauaji hayo Mkoani Shinyanga.
Bi. Telack alisema hayo wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha siku moja na Shirika la Msichana Initiative na Championi wa kutokomeza ndoa za utotoni mkoani Shinyanga kilichowakutanisha baadhi ya wabunge ambao wanaunda kikundi hicho pamoja na wadau wengine waliokutana leo kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Bi. Telack aliongeza kuwa kipindi cha nyuma vyombo vya habari kila kukicha vilikuwa vinaandika sana kuhusu mauaji ya mama wazee waliokuwa wanauawa kutokana na ramli chonganishi lakini sasa hali ni shwari na vyombo vya habari havitoi tena habari za mauaji hayo kwani hayapo tena.
Kuhusu mimba na ndoa za utotoni Bi. Telack alisema kuwa juhudi zilizofanyika ni pamoja na kukamata watoto wakiwa wanafungisha ndoa na juhudi hizo zilifanyika baada ya Mkoa huo kuwa na takwimu za juu kwani awali Mkoa wa Shinyanga uliongoza 59% ya ndoa za utotoni Nchini.
Bi Telack alisema msukumo wa mikakati ya kupambana na mimba na ndoa za utotoni ulitokana na Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii kutoa takwimu hizo kwa Mkoa wa wake wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Mtoto wa Kike yaliyoadhimisha Kitaifa Mkoani Shinyanga mwaka 2016.
Bi. Telack aliongeza kuwa wanaume ambao wamekamatwa kwa kuwapa mimba watoto wa shule wamekuwa wakipata kifungo cha miaka 30 jela pomoja na changamoto ya baadhi ya Wazazi kushawisi watoto wao wasitoe ushahidi mahakamani lakini pia na wasimamizi wa sheria kwa kushirikishwa katika masuala haya kwa sasa hakuna ucheleweshaji kesi hizi.
Bi. Telack amewataka wanaume kutambua kuwa mtoto wa mwenzeke mwenye umri sawa na mtoto wake sio mke kama ilivyo kwa mtoto wake hivyo wawachukulie watoto wa wenzao kama watoto wao na hivyo kukomesha vityendo vya mimba na ndoa za utotoni ili kutoa fursa kuwalinda watoto wakike.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative Bi. Rebeca Gyumi amewaambia wabunge machampioni wa kutokomeza ndoa za utotoni kuwa lengo la kikao hiki ilikuwa ni kuwapa fursa kwao kufahamu juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Shinyanga katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili iwe fursa kwao kutumia uzoefu huo kwa bunge lakini pia katika maeneo yote ya Tanzania.