Morrison Amenoga Simba, Gomes Ampa AS Vita





WAKIWA katika maandalizi ya mchezo wa tano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes amesifu kiwango cha sasa cha kiungo mshambuliaji Mghana Bernard Morrison huku akimpa jukumu zito katika pambano hilo.

 

Simba inayoongoza Kundi A ikiwa na pointi 10 wakifuatiwa na Al Ahly wenye 7, watavaana na AS Vita kesho Jumamosi saa kumi kamili kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Katika mchezo huo, Simba wanahitaji kupata ushindi wowote ili wajiwekee nafasi nzuri ya kumaliza michuano hiyo wakiwa kileleni katika msimamo wa kundi hilo.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Gomes alisema kuwa ameona mabadiliko makubwa ya kiungo wake huyo katika mazoezi yake na kwenye mchezo uliopita wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika walipocheza dhidi ya Al Merrikh.

 

Gomes alisema awali alikuwa hampi nafasi ya kumuanzisha kiungo huyo kutokana na kutokuwa ‘siriasi’ uwanjani huku akileta utani mwingi kabla ya kumuonya na kubadilika hivi sasa.

 

Aliongeza kuwa kama kiungo huyo akiacha masihala ni bonge la mchezaji kutokana na kiwango chake kikubwa cha kutengeneza na kufunga mabao katika mechi.“Mimi sina hofu juu ya uwezo wa Morrison, alikuwa na shida ndogo ambayo nimeifanyia kazi kwa kumtaka abadilike na tayari amefanya hivyo ndiyo sababu ya yeye kuonekana bora na kumpa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza,” alisema Gomes.

 

Aidha, kocha huyo katika mazoezi ya juzi alionekana akimpa program maalum ya jinsi ya kupiga krosi anapolikaribia goli la wapinzani huku akimzuia kupiga chenga.

 

Kiungo huyo alikuwa akipigiwa pasi na Ibrahim Ajibu na Francis Kahata ambao nao walikuwa wakipokea mipira kutoka kwa Jonas Mkude na Mzamiru Yassin.

 

Morrison alitakiwa kukokota mara mbili pekee kabla ya kuwapigia krosi washambuliaji wa Simba Mkongomani Chris Mugalu na John Bocco kwa ajili ya kufunga kipa akiwa Beno Kakolanya.

 

Upo uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kuanza katika kikosi cha kwanza kitakachoivaa AS Vita kutokana na kocha huyo kuonekana kumpa maelekezo maalum nyota huyo katika mazoezi ya juzi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad