Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeshindwa kuhuisha vipengele vyote vya upembuzi yakinifu uliofanyika awali katika ujenzi wa mradi wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), imeeleza ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Badala yake ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 2020 imesema Tanesco lilitegemea upembuzi yakinifu ambao ulifanywa katika miaka ya 1970 na 1972 na kampuni ya M/S Norconsult ya Norway.
Pia shirika hilo linatumia mpango mtambuka wa mradi na ripoti ya uchunguzi wa kiufundi uliofanywa na kampuni ya M/S Hafslund na M/s Norplan pia kutoka Norway ambayo ilihuisha vipengele vya taarifa ya upembuzi yakinifu miaka ya 1980.
“Vipengele ambavyo havikufanyiwa mapitio na kuhuishwa ni pamoja na utafiti wa kiuchumi na kifedha wa mradi, tafiti za kuwepo kwa maji na uendeshaji endelevu wa mradi,” imesema ripoti hiyo.