Upande wa mashtaka katika kesi kuhusu kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd aliyekufa kwa kugandamiziwa goti shingoni na polisi Mzungu, umesema uchunguzi wa kitaalamu umeonesha kuwa Floyd alikufa kutokana na kukosa hewa ya oksijeni.
Shahidi wa upande huo ambaye ni daktari wa mapafu, Martin Tobin, amesema kukosa hewa hiyo ndiko kulikoufanya moyo wa marehemu kusimama, na amekosoa madai ya upande wa utetezi wa polisi anayeshutumiwa kumuuwa Floyd, Derek Chauvin, kwamba magonjwa aliyokuwa nayo George Floyd yalichangia katika kifo chake.
Mkanda wa vidio uliosambaa duniani, ulimuonesha Chauvin akigandamiza goti lake katika shingo ya Floyd kwa muda wa takribani dakika tisa.