Mwakalebela: Natafakari Kukata Rufaa TFF





“HIZO taarifa ndiyo kwanza nazipata kwako, hivyo bado sijajua maamuzi yoyote juu ya hilo, lakini hivi sasa natafakari kama nitaweza kukata rufaa,” hiyo ni kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Lugano Mwakalebela mara baada ya kuulizwa kuhusu kufungiwa kujihusisha na soka.

 

Jana, Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilitangaza kumfungia Mwakalebela kujihusisha na soka ndani na nje ya Tanzania kwa muda wa miaka mitano na kutakiwa kulipa faini ya shilingi 7,000,000, kwa kosa la maadili.

Taarifa iliyotolewa na TFF kupitia kwa Ofisa Habari na Mawasiliano, Clifford Mario Ndimbo ilisema:

 

“Mwakalebela ametiwa hatiani kwa kutoa maneno ya uchochezi kwa nia ya kuchochea mashabiki, wanachama na wapenzi wa Yanga dhidi ya vyombo vinavyosimamia mpira wa miguu nchini.

“Uamuzi huo wa kamati umetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 73(4) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo 2013.

 

”Taarifa hiyo ilizidi kueleza kuwa: “Mwakalebela alilalamikiwa kuwa Februari 19, mwaka huu, aliitisha Mkutano na Waandishi wa Habari na kudai kuwa TFF, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, zinahujumu timu ya Yanga, madai ambayo alishindwa kuthibitisha mbele ya kamati.

 

“Katika shtaka la pili, Mwakalebela alilalamikiwa kwa kutoa taarifa za uongo ambapo Oktoba 1, 2020 aliitisha mkutano na kudai kuwa anao mkataba kati ya mchezaji Bernard Morrison na Klabu ya Simba na kuonesha kwa waandishi wa habari huku akijua ni uongo na kitendo hicho ni kinyume na sheria.

 

“Kamati imemtia hatiani katika shtaka hilo na kumpa onyo la kutotenda kosa hilo kwa muda wa miaka mitano. Pia imemtoza faini ya Sh 2,000,000. Adhabu hizo ni kwa mujibu wa kifungu cha 6 (1) (b) na 6 (1) (c) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.

STORI: ISSA LIPONDA, Dar es salaam

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad