Juma Mwambusi
KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi, juzi aliondoka kikosini humo na kurejea kwao Mbeya kwa ajili ya kuhani msiba wa ndugu yake ambaye alifariki hivi karibuni.
Tangu Mwambusi akabidhiwe mikoba ya Cedrick Kaze amedumu na Yanga kwa takribani miezi miwili kabla ya Jumanne iliyopita kumtambulisha kocha mkuu mpya raia wa Tunisia, Noureddine Al Nabi.
Championi Jumamosi limezungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga, Hassan Bumbuli ambaye ameweka wazi kuwa, “Kocha Mwambusi hawezi kuachana na sisi kwa sasa maana bado ana mkataba unaotarajiwa kuisha Juni 30, mwaka huu.
“Hivyo, kwa wale wanaodhani hatakuwepo kwenye mechi yetu dhidi ya Azam FC, watakuwa wanajidanganya maana hadi jana Alhamisi (juzi) tulikuwa naye kambini na tulifuturu pamoja hadi alipopata taarifa za msiba na kuomba ruhusa kwenda kuhani msiba huo.
“Mbali na hivyo utaona pia kuwa program zote za mazoezi kaendesha yeye na kwamba maelekezo yote ya benchi amemkabidhi yeye, hivyo hadi anaondoka kaacha program ambayo inaendelea kusimamiwa na kocha mkuu hadi yeye atakaporudi hiyo Jumamosi (leo) tayari kwa kukaa kwenye benchi wakati wa mchezo wetu na Azam FC,” alisema Bumbuli.