JESHI la Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na dawa za kulevya (ADU), limewakama watu wanne akiwemo mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu (TIA), Allu Mirumgwa (24) wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 31 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye mabegi mawili.
Tukio hilo limethibitishwa Machi 9, 2021, na Mkuu wa Kitengo hicho, Hassan Kabeleke, ambapo amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Joseph Dalidali(26) mkazi wa Mbezi beach, Said Mbasha (24) mkazi wa Kinondoni na Fatuma Shomari.
Kabaleke amesema wamepokea taarifa hiyo kutoka kwa raia mwema kuwa kuna watu wanajihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya eneo la Mbezi beach na Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Kabaleke ameendelea kusimulia kuwa baada ya kupokea taarifa hizo walipanga timu tatu ya Askari ambapo walianza kufatilia kuanzia Machi 3, mwaka huu huko maeneo ya Mbezi Beach A Mtaa wa Madafu walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Dalidali na alipohojiwa alikiri kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Aidha, Kabaleke amesema Machi 3 mwaka huu majira ya saa 8 mchana walimkamata mwanafunzi wa chuo cha uhasibu, Murungwa akiwa eneo la Kijitonyama na alipekuliwa katika nyumba aliyokuwa amepanga na kukutwa na pakiti 31 zenye uzito wa kilo 30.6 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye mabegi mawili.