Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewataka wafanyabiashara wanaoficha fedha majumbani kuacha kufanya hivyo na badala yake wahifadhi benki kwa sababu haziwezi kuchukuliwa.
Aidha, Dkt. Mwigulu amesisitiza watendaji wa Wizara hiyo kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu kuhusu kupanua wigo wa kodi kwa kuongeza walipakodi wapya huku waliopo wakitakiwa kulindwa ili kukuza uchumi wa nchi.
“Kwa wale Wafanyabiashara ambao walishaanza kuona nikiweka hela yangu ikaonekana mtandaoni labda itachukuliwa yote, nitoe rai warudishe fedha kwenye mabenki, zitaliwa mchwa huko na panya bila sababu.
“Mojawapo ya mambo yanayojitokeza hata katika mijadala mingi bungeni ni ukadiriaji wetu tunaoufanya wa kodi zetu tuufanye kwa kuzingatia sheria na weledi katika sekta hiyo ya ukusanyaji mapato.
“Kuna maeneo ambayo yamekuwa yakijitokeza yanaleta mkanganyiko tuyaache mfano anatokea mtu ameshakadiriwa miaka yote kodi na amepewa ‘clearance’ kwamba huyu tumemkadiria na amelipa inapita miaka kumi anaenda kukadiriwa tena anapigiwa hesabu ya miaka kumi au kumi na tano ambayo katika miaka hiyo yote alipewa certificate.
“Kuna wale ambao wao mara zote wanabadilisha maelekezo nadhani niwape angalizo mapema tu maana yake wakati msisitizo umetolewa kuwa tukusanye kodi wale wengine walikuwa wanaenda wanavamia tu wanasema tumeambiwa tukusanye kodi mpaka mtakoma.
“Sasa hivi watu wataambiwa kusanyeni kwa weledi halafu wataenda waseme sasa hivi ni kula kuku tu nchi hii tutaijenga sisi wenyewe na tutaijenga kwa kodi,” Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba.