UONGOZI wa Klabu ya Yanga umesema kuwa upo kwenye mipango madhubuti ya kufanya usajili mkubwa katika dirisha la usajili la mwezi Juni mwaka huu kwa kuleta majembe mapya ya kazi, na kuwaondoa baadhi ya nyota ambao wanaonekana kuwa na mchango mdogo kwenye kikosi hicho.
Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Yanga ambao inatajwa wapo kwenye hatari ya kuachwa ndani ya kikosi hicho ni washambuliaji Michael Sarpong, Fiston Abdoul Razak na Ditram Nchimbi ambao kwa jumla wao wamefunga mabao sita tu kwenye ligi mpaka sasa.
Katika siku za hivi karibuni Yanga wameonekana kukosa makali, hasa katika safu yake ya ushambuliaji ambapo licha ya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zao 51, kikosi hicho kimepata ushindi mmoja pekee kati ya michezo saba iliyopita imefungwa mechi moja na kutoa sare michezo mitano.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfi kirwa alisema ni lazima klabu hiyo ifanye usajili mkubwa katika dirisha la mwezi Juni, ili kuboresha maeneo yanayoonekana kuwa na mapungufu.
“Ni kweli kama uongozi tunajua wazi kuwa licha ya ubora wa wachezaji tulionao, kikosi chetu kitalazimika kufanya usajili mkubwa katika dirisha la usajili la mwezi Juni, mwaka huu, ili kufanya maboresho katika baadhi ya maeneo ambayo yameonekana kuwa na mapungufu ikiwemo nafasi ya ushambuliaji.
“Tunatarajia kusajili majina mapya makubwa kwenye usajili wa dirisha kubwa, lakini pia tutaachana na baadhi ya wachezaji ambao wanaonekana kutokidhi mahitaji ya kikosi chetu.
“Yanga ni timu kubwa na sifa ya timu kubwa yoyote ni lazima ihakikishe inafanya usajili, hivyo kama uongozi tumejidhatiti katika hilo.”