Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (CCM), Dar amekuja na kampeni ya kuinua somo la Hisabati kwenye jimbo hilo iitwayo ‘Kiu Hisabati Ubungo’ pamoja na kuzindua nembo mpya ya jimbo hilo.
Katika kampeni hiyo Waziri Mkumbo amekuja na ubunifu wa kutoa motisha kwa walimu wa somo hilo na wanafunzi watakaofanya vizuri kwenye jimbo la Ubungo.
Akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa elimu akiwamo Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Ummy Mwalimu, Prof. Kitila amesema kuanzia mwaka huu atatoa motisha kwa walimu na wanafunzi watakaofanya vizuri kwenye somo hilo.
Wadau wakiwa kwenye hafla hiyo.
Profesa Mkumbo amesema amelazimika kulivalia njuga somo hilo kwenye jimbo lake baada ya mwaka jana kufeli kwa kiasi kikubwa na kukosa mwanafunzi hata mmoja aliyepata alama A.
Katika hamasa yake amesema ameandaa Tuzo na cheti kwa walimu wa hisabati watakaofanya vizuri na kupata alama A.
Mbali na tuzo hizo, walimu watakaofanikisha mwanafunzi wake kupata alama A sambamba na mwanafunzi husika, wote watapatiwa pia zawadi ya Sh 100,000.
Kisare Makori akizungumza na wanahabari baada ya uzinduzi wa mpango huo.
Waziri Kitila amesema wanafunzi hao wanakaofanya vizuri kwenye somo hilo na kuchaguliwa kuingia kidato cha tano atawalipia ada pamoja na kuwagharamia sare za shule na mahitaji yao mengine.
Ameendelea kusema kuwa wanafunzi watakaopata B, atawalipia ada ya nusu muhula.
Akielezea sababu ya kulivalia njuga somo la hisabati Waziri Mkumbo amesema somo hilo ndiyo msingi wa masomo yote na kichwa kikishachangamshwa na hisabati kwa masomo mengine kinakuwa ni mepesi kabisa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatris Dominic akimpongeza Profesa Mkumbo kwa ubunifu wake huo wa kulikuza somo la hisabati.
“Yaani kichwa kikipashwa kwa hisabati na masomo mengine ‘automatikali’ nayo yanakuwa mepesi hivyo ndiyo maana nikaona nilikazanie somo la hisabati ambalo matokeo yake kwenye jimbo langu yamenisikitisha sana mpaka nikaamua kuanzisha kampeni hii,’ alisema.
Katika tukio hilo Waziri Mkumbo ametumia nafasi hiyo kuzindua nembo mpya ya jimbo hilo iliyobuniwa na wa jimbo hilo katika shindano maalum ambapo washindi watatu waliobuni vizuri nembo hiyo walizawadia shilingi 100,000 kila mmoja.
Profesa Mkumbo na Ummy Mwalimu wakimpongeza kijana aliyeshiriki kuchora nembo mpya ya Jimbo la Ubungo.
Katika hafla hiyo, Waziri Ummy alimpongeza Prof. Mkumbo kwa ubunifu wake huo wa kuinua elimu nchini na kuwataka wengine kuiga kampeni kama hizo kwenye maeneo yao ili kuinua elimu nchi nzima.
Hii ndiyo nembo mpya ya Jimbo la Ubungo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo,Beatrice Dominick aliyekuwa kwenye hafla hiyo alimpongeza Prof Mkumbo ubunifu wake huo wa kuinua elimu kwenye jimbo hilo lilopo kwenye Manispaa yake na kueleza furaha yake ya kufanya kazi na Mbunge mwenye mikakati ya kimaendeleo kama Prof. Mkumbo.