Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kutanua wigo wa ukusanyaji kodi akionya kile alichokiita kuwaua walipa kodi kwa kufunga biashara zao, kuchukua fedha na vifaa vyao vya kazi pamoja na kufunga akaunti zao.
Samia ameyasema hayo leo, Ikulu Chamwino jijini Dodoma, wakati akiwaapisha Mawaziri, Manaibu Mawaziri pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi aliowateua jana.
Huku akirejea kauli ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyeagiza makusanyo ya Serikali kwa mwezi kuanzia Oktoba mwaka 2021 yaanze kuwa Sh2 trilioni amesema, “nendeni mkatanue wigo wa kodi na mtengeneze walipa kodi wengi zaidi. Trend mnayoenda nayo ni kuua walipa kodi, wafanyabiashara. Mnatumia nguvu kubwa kuwakamua, mnachukua vifaa vyao vya kazi mnakwenda kufungia akaunti zao mnachukua fedha kwa nguvu kwenye akaunti.”
“Akitoka hapo anakwenda kufunga biashara anahamia nchi jirani naombeni sana nendeni mkaongeze walipa kodi yale yanayopunguza walipa kodi mkayasimamie. Tunamaliza Pasaka Jumatatu pengine Jumanne tukaja hapa kuapishana na wengine.”
Kiongozi huyo pia aliwaonya viongozi mbalimbali kuacha kuwekeza katika kampeni za mwaka 2025, badala yake wafanye kazi na kwamba rekodi itaamua wakati ukifika.
“Tunaelekea 2025 huko watu huwa wanakuwa na mengi acheni. Twendeni tufanye kazi hili na lile tutajua mbeleni kwa hiyo rekodi yako inakufuata kwenye maisha yako na mimi nitakuwa makini kuangalia rekodi zenu . Niwaambie kila mwenye nia ya 2025 aache mara moja,” amesema Rais Samia.