Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema jitihada zaidi zinahitajika kukuza uchumi na kupambana na umasikini kwa sababu licha ya mafanikio yaliyopatikana kasi ya ukuaji wake bado ni ndogo.
Amesema wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa ili kupambana na umasikini uchumi unatakiwa kukua angalau kwa asilimia nane kwa mwaka.
Ametoa kauli hiyo Alhamisi Aprili 22, 2021 wakati akilihutubia Bunge mjini Dodoma ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoapishwa Machi 19, 2021 baada ya kifo cha rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kilichotokeza Machi 17, 2021.
Samia amebainisha kuwa kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, uchumi duniani umeshuka na Tanzania ni miongoni mwaka nchi hizo akisema umeshuka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 4.7.
“Hii inamaanisha kuwa katika miaka mitano ijayo tunahitajika uwekezaji mkubwa sana katika sekta za uzalishaji na zinatoa ajira kwa wingi,” amesema Samia.
Amesema hatua mahsusi zitakazofanyika katika kukuza uwekezaji ni kufanya marekebisho katika sera, sharia, kanuni na kuondoa vifungu vinavyobainika kusababisha vikwazo katika kukuza uwekezaji.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sera za uchumi wa jumla na sera za fedha kuhakikisha viashiria vya uchumi, ikiwemo thamani ya sarafu, mfumuko wa bei na viwango vya riba vinabaki katika hali ya utulivu.
“Sambamba na hilo hatutakuwa tayari kuvumilia uvivu, uzembe, wizi na ubadhilifu wa mali au fedha za umma. Tutachukua hatua madhubuti kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuivutia sekta binafsi kushiriki vizuri kwenye shughuli za kiuchumi,” amesema Samia.
Amesema mwelekeo utakuwa kurudisha imani ya wawekezaji na kutoa vivutio kwa wawekezaji mahiri ikiwa ni kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa haraka.
“Ndani ya nchi yetu kumekuwa na mzunguko mkubwa watu wanapokuja kutaka kuwekeza, Serikali ya awamu ya sita inakwenda kukomesha hilo na uwekezaji sasa utakwenda kufanyika kwa haraka,” amesisitiza.