MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge, leo Aprili 18, amefanya ziara ya kukagua miradi minne ya maendeleo iliyopo katika mkoa huo ambapo amemtaka Mkandarasi kutoka kampuni ya JASCO anayejenga barabara ya Makongo kuhakikisha inakamilika kabla ya Mwezi Octoba.
RC Kunenge amezitaka Taasisi za DAWASA na TANESCO kufanya kazi kwa ushirikiano na Mkandarasi huyo kwa kuondoa miundombinu ya maji na umeme iliyopita kwenye mradi ili Mkandarasi asipate changamoto yoyote kukamilisha mradi.
Kunenge amesema barabara hiyo yenye urefu wa KM 4.5 ni moja ya barabara muhimu Katika kutatua changamoto ya foleni kwenye barabara ya Bagamoyo ambapo mradi huo umegharimu zaidi ya bilioni 8.2.
Pia, Kunenge ametembelea ujenzi wa barabara ya Madale kuelekea Wazo yenye urefu wa KM 6 inayogharimu shilingi bilioni 9.7 ambapo amemuelekeza Mkandarasi kutoka kampuni ya MECCO kukabidhi mradi mwezi wa tano mwishoni Kutokana na barabara hiyo kuwa msaada mkubwa kwa mabasi yaendayo Mikoa ya kaskazini yakitokea Kituo cha mabasi cha Magufuli.