Na Ahmad Mmow, Lindi.
Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) mkoa wa Lindi imewafikisha mahakamani viongozi wa chama cha msingi cha ushirika (AMCOS) cha Stesheni, wilaya ya Nachingwea kwa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi 84,741,200.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya TAKUKURU ya mkoa wa Lindi iliyopo mjini Lindi. Mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Lindi, mhandisi Abnery Mganga alisema TAKUKURU kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya mashitaka, leo imewafikisha mahakamani viongozi watatu wa AMCOS ya Stesheni kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa shilingi 84,741,200. Ambapo uchunguzi wa tuhuma hiyo umekamilika na tayari mkurugenzi wa mashitaka ameshatoa kibali cha viongozi hao kushitakiwa.
Mhandisi Mganga aliwataja viongozi hao ambao wameshitakiwa katika mahakama ya wilaya ya Nachingwea kuwa ni Kassim Nnandaje, Said Ismali na Santos Issa.
Ofisa mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Lindi alisema tarehe 2.10.2012 wilayani Nachingwea TAKUKURU wilayani humo ilipokea taarifa ya ubadhirifu wa kiasi hicho cha fedha(shilingi 84.74 milioni) ambazo zilitolewa kwenye akaunti ya chama hicho kwa awamu mbili. Fedha ambazo zilitakiwa zitumike kuwalipa wakulima wa korosho katika msimu wa 2011/2012.
Alisema taarifa za siri zilieleza kwamba ingawa fedha zilitolewa kwa ajili ya malipo ya wakulima, hata hivyo kiasi kilicho salia baada ya malipo hakijulikani kilipo.
Mhandisi Mganga alibainisha kwamba baada ya kupokea taarifa hizo TAKUKURU wilaya ya Nachingwea ilianza uchunguzi kwa lengo la kubaini na kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo. Ambapo ilijiridhisha kuwa nizakweli na kubaini kwamba katika awamu ya kwanza zilitolewa shilingi 590,450,000 kwaajili ya kuwalipa wakulima wa korosho malipo ya korosho zenye uzito wa kilo 671,424 ambazo zilinunuliwa kwa shilingi 850 kwa kila kilo moja.
Alisema viongozi hao licha ya kutumia shilingi 570,710,400 kwa kuwalipa wakulima lakini kiasi cha shilingi 19,739,600 ambacho kilisalia hakikurejeshwa benki.
'' Ilibainika katika uchunguzi wetu kuwa awamu ya pili watuhumiwa walitoa shilingi 300,000,000 kutoka kwenye akaunti ya chama hicho ili wawalipe wakulima. Jumla ya shilingi 234,998,400 walilipwa wakulima. Hatahivyo shilingi 65,001,600 ambazo zilisalia hazikurejeshwa kwenye akaunti,'' alisema mhandisi Mganga.
Mkuu huyo wa TAKUKURU ambaye alisema kitendo hicho ni makosa kwa mujibu wa sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007 aliweka wazi kwamba baada ya kukamilisha uchunguzi huo jalada lilipelekwa kwa mkurugenzi wa mashitaka kwaajili ya kuomba kibali cha kuwashitaki mahakamani. Kibali ambacho mkurugenzi wa mashitaka ameshotoa na kusababisha viongozi hao kufikishwa mahakamani leo (17.4.2021).
'' Watu hao ili kutimiza nia yao ovu waliandaa taarifa za malipo ya uongo kwamba fedha zote zilizotolewa zilitumika kuwalipa wakulima, jambo ambalo siyo la kweli,'' Mganga alibainisha.
Mganga ambae pia aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU alisema viongozi hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni ubadhirifu wa mali ya umma na kula njama kutenda kosa.