Bunge la Jamhuri ya Mungano wa Tanzania leo Jumatatu tarehe 12 Aprili, 2021 limepitisha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 hadi 2025/26.
Mpango huo utakaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 114.8 umepangwa kutekeleza maeneo makuu matano ya kipaumbele, ikiwemo kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma.
Vipaumbele vingine ni kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.
" Tutahakikisha kwamba miradi yote ya kimkakati iliyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano itatekelezwa kama ilivyopangwa", alisema Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakati akihitimisha mjadala kuhusu Mpango huo Bungeni jijini Dodoma.
Shabaha ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 hadi 2025/26 ni pamoja na kupandisha kiwango cha ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 6.0 ya mwaka 2021 hadi kufikia wastani wa asilimia 8.0 itakapofika mwaka 2026.
Aidha mfumuko wa bei umebashiriwa kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja kwa wastani wa asilimia kati ya 3.0 hadi 5.0 katika kipindi cha muda wa kati na akiba za kigeni kukidhi mahitaji ya uagizaji wa huduma na bidhaa kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Malengo mengine ni kuhakikisha kuwa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri yanaongezeka kutoka asilimia 15.9 ya pato la Taifa mwaka 2021/22 hadi asilimia 16.8 itakapofika mwaka 2026 na sekta binafsi inatarajiwa kuzalisha ajira mpya zipatazo milioni nane kati ya Julai 2021 na Juni 2026.
Miongoni mwa viongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, waliohudhuria uhitimishaji wa mjadala huo wakiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ni Naibu wake Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) pamoja na Manaibu Katibu Mkuu Bi. Amina Khamis Shaaban na Bw. Adolf Ndunguru na baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo.