Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere leo Aprili 8, 2021 ameisoma ripoti yake ya mwaka wa fedha 2020/21 mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma.
Katika ripoti yake hiyo ambayo Machi 28, 2021 aliikabidhi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amebainisha kuwepo kwa malipo yaliyofanywa nje ya bajeti na taasisi mbalimbali zikiwemo wizara.
''Katika ukaguzi wa mwaka huu nilibaini kuwa malipo ya zaidi ya Shilingi Bilioni 29 yalifanyika nje ya bajeti. Baadhi ya taasisi zilizofanya malipo nje ya bajeti ni Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, TANROADS, Shirika la Uzalishaji mali la Magereza, TAWA, TARURA, TIA, UNESCO, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkoa wa Songwe,'' ameweka wazi CAG Charles Kichere.
Aidha ameongeza kuwa, "Katika ukaguzi nilibaini kuwa wakala wa ndege za Serikali (TGFA) ililipa bilioni 3.92 ikiwa ni gharama ya huduma za matengenezo makubwa ya ndege hata hivyo baada ya ziara yangu nilibaini ndege haikuwa ikifanya kazi na ilikuwa imetelekezwa tangu 2015,".
Kwa upande mwingine ameeleza juu ya kufanyiwa kazi kwa mapendekezo ya miaka iliyopita ambapo amesema, "Kati ya mapendekezo 8440 yaliyotolewa miaka iliyopita, mapendekezo 2610 yametekelezwa kikamilifu, 2662 utekelezaji unaendelea, 2292 utekelezaji wake haujaanza, 751 yamerudiwa, 426 utekelezaji wake umepitwa na wakati".