Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo Ijumaa limeshusha rungu zito kwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kwa kumfungia kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano.
Mwakalebela pia ametozwa faini ya Sh5 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kutoa maneno ya uchochezi kwa nia ya kuchochea washabiki, wanachama na wapenzi wa Yanga dhidi ya vyombo vinavyosimamia mpira wa miguu nchini.
Uamuzi huo umetolewa na kamati ya maadili ya TFF kwa kuzingatia kifungu cha 73(4) cha kanuni za maadili za TFF toleo la 2013.
Mwakalebela alilalamikiwa kuwa Februari 19 mwaka huu aliitisha mkutano na Waandishi wa Habari na kudai kuwa TFF, Bodi ya Ligi Kuu Tazania Bara (TPLB) na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa ligi hiyo zinaihujumu Yanga, madai ambayo alishindwa kuthibitisha mbele ya kamati.
Katika shtaka la pili, Mwakalebela alilalamikiwa kwa kutoa taarifa za uongo ambapo Oktoba 1, 2020 aliitisha mkutano na kudai kuwa anao mkataba kati ya mchezaji Bernard Morrison na klabu ya Simba na kuuonesha kwa Waandishi wa Habari huku akijua ni uongo na kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Kamati ya maadili imemtia hatiani katika shtaka hilo na kumpa onyo la kutotenda kosa hilo tena kwa muda wa miaka mitano. Pia kamati imemtoza faini ya shilingi 2 milioni (2,000,000) na adhabu hizo ni kwa mujibu wa kifungu cha 6(1) (b) na 6(1) (c) cha kanuni za TFF toleo la 2013.