MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa mpya leo Aprili 25, kuwa mwenendo wa Kimbunga hafifu Jobo unaonesha kuwa katika kipindi cha saa sita zilizopita Kimbunga Jobo kimepoteza nguvu yake wakati kikiingia Nchi kavu kusini mwa Mkoa wa Pwani na Dar Es Salaam usiku wa April 24, 2021.
Hali hii ilisababishwa na kuendelea kuimarika kwa upepo kinzani katika mwelekeo wa Kimbunga hicho, mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na Kimbunga hicho yamesambaa Baharini karibu na maeneo ya kusini mwa Pwani ya Tanzania na Msumbiji.
Kwa sasa, Kimbunga hafifu Jobo hakipo katika Nchi yetu na hakuna madhara ya moja kwa moja yanayotarajiwa, hata hivyo masalia ya mawingu yanayoambatana na kilichokuwa kimbunga Jobo yanaweza kusababisha mvua katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Pwani.
Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika.