Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kimbunga Jobo kimepungua nguvu kwa haraka baada ya kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa upepo kinzani.
Taarifa iliyotolewa na TMA leo Jumamosi Aprili 24, 2021 imeeleza kuwa kimbunga hicho kimekuwa hafifu na kinasafiri kwa kasi ya kilometa 18 kwa saa baharini tofauti na spidi ya kilometa 60 kwa saa iliyokuwa imetabiriwa awali.
TMA imesema kimbunga hicho kilichopo Bahari ya Hindi kwa sasa kipo umbali wa kilomita 200 mashariki mwa kisiwa cha Mafia.
“Kimbunga hafifu cha Jobo kinatarajiwa kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika maeneo machache hususan ya ukanda wa Pwani kadri kinavyosogea nchi kavu kwa siku ya leo Aprili 24 na kesho Aprili 25, 2021,” inaeleza taarifa hiyo.
Maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikiwemo kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja.
Aidha TMA imetahadhalisha kuwa uwepo wa kimbunga hafifu baharini, unatarajiwa kusababisha mawimbi makubwa.