Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema Aprili 25, 2021 Kimbunga Jobo kitapiga mkoani Dar es Salaam kikiambatana na upepo mkubwa wa kilometa 60 kwa saa na kuleta madhara.
Mbali na Dar es Salaam, mikoa mingine itakayoathiriwa na kimbunga hicho ni Mtwara, Lindi, Pwani, Unguja, Zanzibar eneo la Ziwa Victoria ambalo halitakuwa na athari ya moja kwa moja.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Aprili 23, 2021 na mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Agness Kijazi akibainisha kuwa kwa sasa kimbunga hicho kipo kilometa 236 kutoka kisiwa cha Mafia kilichopo mkoani Pwani.
Amesema hadi Aprili 24, 2021 kimbunga hicho kitakuwa kilometa 126 kutoka kisiwa cha Mafia na Aprili 25, 2021 kitafika Dar es Salaam kadri mwelekeo unavyoonyesha.
"Kulingana na ukubwa wa hiki kimbunga cha Jobo kina nguvu kadri kinavyosogea nguvu yake inapungua lakini bado nguvu hiyo ni kubwa inaweza kuleta athari kwa sababu sasa hivi nguvu yake ni kilometa 90 kwa saa.”
"Lakini tunatarajia kwa kesho upepo utakuwa kilometa 70 kwa saa wakati kinatua Dar es Salaam kitakuwa kilometa 60 kwa saa ambao ni upepo mkubwa na unaweza kuleta athari. Sasa hivi kimeanza kushuka kinaenda kwa mwendo kasi kilometa 12 kwa saa lakini kinasogea tahadhali ichukuliwe kwa ukanda wa Pwani," amesema DK Kijazi.