NGUMU kuamini lakini ndiyo hivyo, Yanga imetajwa kuwa iko mbioni kumsajili beki wa kushoto wa Simba, Hussein Mohammed ‘Tshabalala’.
Nyota huyo ni kati ya wachezaji wanaomaliza mikataba ya kuichezea timu hiyo kwenye msimu huu ambaye yeye inadaiwa amebakisha mwezi mmoja.Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mchezaji anapobakisha miezi sita, anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayomhitaji, hivyo Tshabalala yupo huru.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kutoka ndani ya Simba beki huyo anachukua maamuzi ya kuondoka kwenye timu hiyo baada kutokuwepo mazungumzo yoyote kati yake na mabosi wake wakati mkataba ukielekea ukingoni.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Yanga imefikia maamuzi ya kutaka kumsajili beki huyo kwa dau kubwa kwa ajili ya kuiboresha safu yao ya ulinzi ya kushoto baada ya kumkosa beki wa aina yake kwa kipindi cha misimu miwili tangu aondoke Gadiel Michael.
Aliongeza kuwa mabosi wa Yanga walioingia vitani kwa ajili ya kufanya usajili kabambe katika kukiimarisha kikosi chao katika msimu ujao ambao huenda wakashiriki michuano ya kimataifa Afrika.
“Yanga imeonekana kudhamiria kufanya usajili kabambe katika msimu ujao ni baada ya mabosi wao GSM ambao wanasimamia usajili kuingia vitani katika kufanikisha usajili wao kwa kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji.
“Kwa kuanzia imepanga kupiga pigo kubwa Msimbazi kwa kumng’oa beki wao wa pembeni Tshabalala ambaye hivi sasa ni kati ya mabeki bora wa pembeni katika ukanda huu wa Afrika.
“Kwa misimu miwili Yanga imemkosa beki wa kushoto wa kiwango cha juu wa aina ya Tshabalala, hivyo mabosi wa Yanga wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa Tshabalala kwa dau kubwa ambalo huenda likavunja rekodi katika usajili wa msimu ujao kwa wachezaji wazawa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes hivi karibuni alizungumzia hatma ya wachezaji wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu na kusema: “Sitakubali kumuachia mchezaji yeyote aliye katika mipango yangu.
“Nafahamu wapo baadhi ya wachezaji muhimu wanaomaliza mikataba yao, lakini ni mapema kulizungumzia hilo la usajili kwani hivi sasa nguvu zetu tumeelekeza katika michuano ya kimataifa.